Akanusha polisi kusindikiza masanduku ya kura

MSIMAMIZI wa Uchaguzi Halmashauri ya Wilaya ya  Ngorongoro, Murtallah Mbillu amekanusha taarifa polisi kusindikiza masanduku ya kura zilizopigwa.

Mbillu ametoa taarifa hiyo leo kwa vyombo vya habari na kusema kuwa taarifa hiyo si ya kweli na ina lengo la kudanganya wananchi na kuleta taharuhi zisizo na sababu.

Amesema taarifa sahihi ni kuwa wakala wa Chama cha Demokrasia Maendeleo (Chadema )ambaye alitakiwa kuwa katika kituo cha kupigia kura cha Ndoinyo kijiji cha Nasiporion, Kata ya Endulen, Tarafa ya Ngorongoro, Wilaya ya Ngorongoro saa mbili asubuhi wakati wa kufungua kituo yeye alifika akiwa amechelewa bila taarifa yoyote.

Amesema kwa vile muda wa kufungua kituo ili wananchi waanze kupiga kura ulishafika upigaji kura ulianza na alipofika ndipo akaanza kupiga picha na kuzituma anakofahamu yeye na waliotumiwa wakatengeneza taarifa hiyo ya uongo wakiwa na lengo wanalolijua wao.

Aidha amesema hadi  sasa hali ni shwari zoezi la upigaji kura linaendelea, mawakala wa Chadema na wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) wapo wakiendelea na uangalizi pia msimamizi na mwangalizi wa uchaguzi  wapo ili kuhakikisha kuwa zoezi la upigaji kura katika kituo hicho linakuwa la huru na haki.

Hivyo ametoa rai kwa umma  kupuuza taarifa hiyo kwani mgombea atakayeongoza kwa wingi wa kura zilizopigwa na wananchi waliojiandikisha katika kituo hicho ndiye atakayetangazwa kuwa mshindi bila kujali ni wa chama gani

Habari Zifananazo

Back to top button