Al Ameen Foundation yasaidia wenye ulemavu

DAR ES SALAAM; TAASISI  ya Al  Ameen Foundation yenye makao makuu Kijitonyama, Dar es Salaam imetoa msaada wa vitimwendo 50 kwa ajili ya watu wenye ulemavu.

Msaada huo ulikabidhiwa hivi karibuni kwa Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeir Bin Ally, tukio lililofanyika makao makuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Kinondoni, Dar es Salaam.

Advertisement

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Mwenyekiti Mtendaji wa Al  Ameen Foundation, Gharib Nassoro Monero, amesema msaada huo wameukabidhi kwa kushirikiana na taasisi ya Goreeb Yateem Trust Fund ya Uingereza.

“Al Ameen Foundation kwa kushirikiana na Goreeb Yateem Trust Fund  tunakabidhi msaada huo wa vitimwendo kwa ajili ya watu wenye ulemavu.

“Uhitaji ni mkubwa hivyo tunakaribisha wadau wengine kusaidia vitu mbalimbali, wanaweza kuwasiliana nasi kwa namba za simu 0715 800 772 au  0657 277747, ama wafike ofisini kwetu Kijitonyama kwa ajili ya vitu mbalimbali vya kusaidia jamii,” amesema Monero wakati wa makabidhiano hayo.

Kwa upande wake Mufti Zubeir amezishukuru taasisi hizo kwa msaada huo na kusema kuwa ni hatua nzuri katika kusaidia jamii na kuwataka wengine kuiga mfano huo.