Alhaji Tambaza na yasiyojulikana Uhuru wa Tanganyika

ILIKUWAJE, ilianzaje na vipi ikawezekana kuufikia uhuru nyuma ya utawala wa kikoloni wa Uingereza?
Safiri nami ndani ya boti hii, hadi Toangoma, Temeke Dar es Salaam. Mwenyeji wangu ni Ahaj Abdallah Mohamed Tambaza, Mstaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki aliyeshiriki siku ya sherehe ya uhuru.
Leo Jumatatu Desemba 9, 2024 tunaadhimisha miaka 63 ya Uhuru, tangu Tanganyika ipate Uhuru kutoka kwa Uingereza Desemba 9, 1961.
Kwa nini tulihitaji Uhuru?
Pengine msomaji unaweza kuwa miongoni mwa Watanzania wengi waliozaliwa baada ya Uhuru, au hata vijana wa kizazi cha sasa ambao wanaweza kujiuliza kwa nini tulitaka Uhuru?
“Nashukuru kwa ugeni wa watu wa aina yenu kuja kwetu huku shamba (anatania) maana saa kama hizi huwa nalala tu au natazama mpira tu:
“Tulipopata Uhuru nilikuwa kijana mdogo wa miaka 12 ama 13, nilikuwa nasoma Shule ya Mnazi Mmoja, jirani tulikuwa tukitazamana na ilipokuwa ofisi ya (TANU) Tanganyika African National Union pale tulikuwa tunaona viongozi mbalimbali kama Mwalimu Nyerere, Oscar Kambona, Mzee Jumbe Tambaza na wengine wengi.
“Hatukuwa tukielewa nini kilikuwa kinaendelea pale. ile nyumba ya Lumumba (ilipokuwa ofisi ya Chama Cha TANU) maana ilikuwa ya miti iliyojengwa mwaka 1929 na Chama Cha Tanganyika African Association (TAA) chini ya Mzee Sykes na watoto wake, pia walikuwemo akina Dossa Aziz, Mzee Rupia, Juma Abdulkadir,” anaelezea Alhaji Abdallah Tambaza akijibu ilivyokuwa na kwa nini tulidai uhuru.
“Kama Wakoloni wangelikuwa watu wazuri, tusingeliwadai uhuru,” anaeleza akitolea mfano kuwa kulikuwa na madaraja ambayo yanatofautisha nani apate nini kwa mlengo wa ‘asili ya watu’.
“Daraja namba moja ni Wazungu, mambo yao yalikuwa tofauti. Walikuwa na maeneo yao ya kukaa ambayo huwezi kukaa huko. Walikuwa na shule zao, hospitali zao.
“Mfano Hospitali ya Ocean Road iliitwa European Hospital, ambayo ilikuwa ikitibia wazungu tu.
“Wahindi walikuwa na Aga Khan ambayo ilikuwa ikiwatibia wao, pia Hindu Mandal ambayo ilikuwa ikitibia Mabohora na Wahindu (jamii za Wahindi),” anasema na kuongeza:
“Waafrika walikuwa wakitibiwa wapi? Hakuna. Walikuwa wazee tu wanatibiwa hapa na pale, chukua mzizi huu, ponda kile unywe, ila baadae tukaja kupata hospitali iliyojengwa na Mzee Sewa Haji.
“Mzee Sewa Haji huyu ni tajiri ambaye aliona watu wakipata tabu. Akajenga Hospitali ‘pale nyuma ya traffic police’ (Barabara ya Sokoine, Dar es Salaam), ambayo aliijenga na kuikabidhi kwa serikali ya kikoloni iwatibie Waafrika,” anasema.
Anasema, hospitali hiyo haikuwa na huduma za viwango ‘ilikuwa ya daraja ya chini’ hakuna vipimo pia hakukuwa na huduma ya kujifungua.
Anasema walikuwepo madaktari lakini gharama zipo juu kama Dk. Chakera, Dk. Lawrance na Dk. Khan.
Ujio wa Princess Margaret/ujenzi wa Muhimbili
“Kufikia 1956, alikuja Princess Margaret kuzuru nchini, ambapo kulikuwa na kelele nyingi kuhusu huduma za afya na hospitali za matabaka.
“Mwaka 1956-57 ikafunguliwa Hospitali ya Muhimbili, ambayo haikuwa na huduma ya kuzalisha. Wakunga walikuwa wanahusika na kazi hiyo.
“Watu wengi walikufa. Life span yetu ilikuwa miaka 35. Watoto walikufa sana. Hilo likasababisha kudai Uhuru,” anaeleza huku akisisitiza kuwa halikuwa jambo jepesi.
Matabaka kwenye makazi
“Kuhusu Wazungu wao walijengewa Oysterbay, ambayo sasa mnaita Masaki, lakini kule sio Masaki. Masaki yenyewe ipo Wilaya ya Kisarawe,” anasema jina la Masaki kulikuwa na Mtaa Oysterbay kwenye kituo cha gari ndipo palitambulika hivyo.
“Majina mengi yameharibiwa, mfano mjini panaitwa Posta lakini kule ni Uzunguni sio Posta,” amesema.
“Babu yangu na rafiki yake walimiliki Upanga karibu yote na Kivukoni,” amesema isivyo bahati Wazungu waliwataka wazee wao waondoke Upanga, ili wawapishe Wahindi daraja la pili.
“Wamegombana sana wazee wale kugombania maeneo yao,”
“Kwa kuwa hawakuwa na chaguo, wazee wale walilazimishwa kuondoka na wakawapa fidia kidogo, ambapo walihama na kwenda kununua Kariakoo, Kisutu kwenye Makaburi, DIT,” amesema na kuongeza:
“Mambo haya hayakuwa yakiwapendeza Waafrika. Kuishi vibanda mbavu vya mbwa, kulalia vibatali nakadhalika. TANU ilipokuja ikashawishi watu kuungana ili kupambania haki zao.”
ELIMU
Shule za serikali zilitolewa kwa matabaka, mfano Azania na Jangwani asili yake ‘Azania Government African Secondary School’ ‘Jangwani Girls African Secondary School’
Watu weusi walisoma ‘Mchikichini African Boys Primary School’
“Wahindi ‘Shia’ walikuwa na shule zao kama Agakhan Boys and Girls ambayo sasa ni Shule ya Muhimbili. Baniani shule yao ilikuwa Kisutu na Bohora shule yao ni Jamhuri Primary School
“Nimeingia Shule darasa la kwanza mwaka 1958. Tuliingia darasani tukiwa pekupeku. Wahindi na Wazungu wao walivaa viatu.
“Chakushangaza walimu wetu wa kiafrika walitukataza tusivae viatu. Tuliungua jua, tuliugua sana kwa ugonjwa wa kichocho,” amesema Walimu wa Kiafrika walitwambia ‘Ninyi mnavaa viatu, mnajidai baba zenu wana uwezo eh?’ Anaelezea kwa uchungu huku akisema hivi ndivyo namna wakoloni walifanya hata Watanzania wasijithamini wenyewe.
Wahuni walivyolinda miji kudai uhuru
“Watu wakaingiwa na hamu kubwa ya kupata uhuru kwa kuwa waliamini, Waafrika watachukua daraja la juu la Wazungu na Wahindi, itakayowawezesha kupata uhuru, kama ilivyoeleza ilani ya TANU.
“Wakati huo Zaire nao walikuwa wakidai Uhuru, ambapo harakati za Wazaire zilikuwa kali kiasi cha kuuwa wakoloni,” anasema jambo hilo lilisababisha Wakoloni wa Tanganyika kunuia kusitisha harakati za kudai uhuru nchini, kwa hofu ya kuuawa kama walivyouawa wakoloni wa Zaire.
Viongozi wa Tanganyika wakawahakikishia viongozi wa kikoloni kuwa hawatowafanyia ‘kuwauwa’ kama walivyofanyiwa watawala wa kikoloni wa Zaire.
Anasimulia kuwa maafikiano hayo yakaibua ari mpya na mikakati ya kupambania Uhuru kwa kuzingatia maafikiano ya amani na kutokumwaga damu.
“Kilichotokea vijana ‘wa kihuni’ walijitolea kulinda miji pamoja na watawala wa wakoloni. Jambo hilo lilifanyika kwa siri na lilifanikiwa.
“Sikuwahi kuona hamasa na mkusanyiko mkubwa kama siku hiyo ya kupata uhuru,” anasema.
“Kulikuwa na kila aina ya ngoma unayoijua wewe. Mimi mara yangu ya kwanza kuona ngoma ya Kimaasai ilikuwa siku hiyo,” anaeleza huku akicheka na kuongeza:
“Nakumbuka, kwa mara ya kwanza, Uwanja wa Uhuru ulitumika siku ya Uhuru ingawa Uwanja wa Karume ulikuwa tayari ukitumika,” amesema.
“Watangazaji mahiri kipindi hicho wa TBC walikuwa Hamza Kasongo, David Wakati, Selemani Hega, Gumbo, Steven Mlatie na wengine.
MATUKIO YALIYONASIBISHWA NA UHURU
Kushusha na kupandisha bendera Uwanja wa Uhuru
Nyirenda alipandisha bendera kwenye Mlima Kilimanjaro
“Mtanzania mmoja mwenye asili ya India, Habibu Punja alituvalisha viatu watoto wote wa Shule wa Dar es Salaam tuliokuwa tukifanya parade kuelekea Uwanja wa Uhuru. Hiyo ni mara ya kwanza kuruhusiwa kuvaa viatu shuleni,” anasema.
“Ilipofika saa 5:50 usiku wa Desemba 08, 1961 tulimuona Ally Kashmir na bwana mmoja ambaye jina limenitoka. Walipita kikakamavu ‘majestically’ kuelekea kwenye bendera ya Uingereza kisha tukamuona Mume wa Malkia wa Uingereza anakuja baadae tukamuona Mwalimu Nyerere naye anakuja.
“Ilipotimu saa 6 kasoro dakika 3 au 4 tukamuona Mwalimu Nyerere na mkewe akiwa mdogo mdogo.
“Hakulala mtu siku hiyo, bendera ilipokuwa ikipandishwa ulikuwa unapigwa ‘Mungu Ibariki…” wimbo wa Taifa anaimba…, siku kadhaa kabla ya uhuru tulifundishwa nyimbo hizo.
“Sherehe za Uhuru zilikuwa za aina yake, haikupata kutokea! Nchi za Mataifa kadhaa zilikuja kucheza nasi kama Ghana, Ethiopia na nyingine.
“Watoto wa shule tuliocheza paredi hatukulipwa lakini tulikabidhiwa vyakula ‘lunch box’,” anasema.
“Ilipofika saa 8 usiku watu wakawa wanaombea kukuche ili wakaishi maghorofani, wasiwe tena ‘maboi’. Watu waliamini vitu vya wahindi vitakuwa vyetu,” anasema.
Anasimulia kuwa, wale wahuni waliokuwa wakilinda miji kipindi chote cha sherehe ya kukabidhiwa uhuru, walifanikiwa kwa kiasi kikubwa, ambapo baadaye walipewa kazi ‘gate keepers’ walinzi, baadhi wakawa askari wa Rais na kazi nyingine za ulinzi na usalama.
MCHANGO WA BAADHI YA WATU KATIKA KUDAI UHURU
John Rupia alitoa kiasi kikubwa cha fedha
“1954 ilipokuja kuwa TANU. Mzee John Rupia alikuwa mtu wakwanza kumlipa Nyerere mshahara Sh 600. John Rupia alikuwa Makamu wa Rais wa TANU nyuma ya Mwalimu Nyerere.
“Aliletwa Zuberi Mtemvu ili aje kuwa Katibu Mkuu wa kwanza wa TANU. Muda huo chama hiki kilikuwa hakifahamiki, hivyo nafasi hizo zilikuwa zikidharaulika sana,” anasema na kuongeza kuwa Mtemvu alikuwa mzungumzaji mzuri kwenye kujenga hoja.
“Baadae alipoanzisha chama chake aliongoza katika kura za Kanda ya Ziwa katika uchaguzi wa urais wa Tanganyika,” anasema na kuongeza:
“Rashid Kawawa, alikuwa Katibu Mkuu wa vyama vyote vya wafanyakazi ‘Tanganyika Federation of Labour’ ilihusisha wafanyakazi wa ndani, wafanyakazi wa bandari, walimu na wafanyakazi wengine wadogo wadogo, ingawa Kawawa, alichelewa kuingia TANU.”
HATUA BAADA YA UHURU
Kisa cha Mtaa wa Vijana, Mwinyijuma na Mwananyamala Hostel:
“Siku moja tulikuwa shuleni Mnazi Mmoja, alishuka Rehema Kawawa akiwa ni Mtoto wa Waziri. Aliletwa na gari ya Kiingereza ‘Hamber’. Tukiwa ‘assemble’ mstarini. Kidogo ilitupa moyo wa kuwa sasa tunaenda kuwa namba moja.
“Ilipitishwa kampeni za kutaifisha majengo kwa kutumia usajili wa majengo ‘building registry’ baadaye NHC (Shirika la Nyumba la Taifa), ambayo iliwapa nafasi Waafrika kuishi ghorofani, na Wahindi walipaswa kulipa kodi ya pango.
“Katika kutekeleza Ilani ya TANU kuwafanya Waafrika wawe na makazi mazuri, hatuwezi kudharau mchango wa Mzee Mwinyijuma Mwinyikambi wa Kitembe aliyekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Kamati Kuu ya TANU, ambaye alikuwa akimiliki mashamba makubwa jijini Dar es Salaam, kuanzia Kinondoni Mkwajuni, Kinondoni Studio na Mwananyamala yote lilikuwa eneo la shamba lake. Alikuwa na mifugo mingi.
“Siku moja alitoa tamko kwamba shamba lake lote analitoa kama zawadi kwa TANU ili zijengwe nyumba bora za kisasa, ili watu weusi waliokuwa wakiteseka wapate makazi bora.
“Hilo likawa chimbuko la ‘National Housing’ (NHC). Hapo ndipo nyumba za tofali kwa watu weusi zilipoanza. Ujenzi uliendelea na baadaye nyumba zikaja kujengwa Magomeni na Ilala.
“Nyumba ziliuzwa Sh 9,000 tu. Unalipia kidogo kidogo baada ya hapo unapewa hati,” amesema.
Vijana walitakiwa watumike kuzalisha matofali ya kujengea ndipo jina Vijana likapatikana.
KUTOKUWA NA SHEREHE ZA UHURU
“Kujikumbushia kumbushia Uhuru si jambo zuri kwa kuwa ni jambo linalouma ‘ni mambo hasi’, kwa hiyo uamuzi wa wakati mwingine kutokuwa na sherehe si jambo baya.
“Mimi binafsi ‘nacriticise’ watu wanaosema sisi Manchester, sisi Chelsea hamtoki leo. Mtaona leo Old Traford,” amesema na kueleza kuwa hali hiyo kwa wao walioona harakati za kudai Uhuru si si sahihi