Aliyefariki miaka 5 iliyopita yadaiwa aonekana akiwa hai

MWASHI Lutema(33), ambaye inadaiwa alifariki dunia miaka mitano iliyopita, ameonekana katika Kijiji cha Kamalampaka kilichopo Wilaya ya Mlele mkoani Katavi.

Tukio hilo limezua taharuki kwa watu wengi, huku ndugu wa mwanamke huyo wakidai ndugu yao alifariki dunia Aprili 2018, baada ya kusumbuliwa na maradhi ya kifua kwa muda mrefu.

Akizungumza na HabariLEO shemeji wa mwanamke huyo, Elias Maduhu amesema kabla ya kifo chake, shemeji yake aliumwa homa na alipozidiwa walimpeleka kwa mganga wa kienyeji kwa matibabu zaidi na ndipo alifariki dunia.

Advertisement

“Baada ya kufariki tulifanya mazishi, ambapo wakati wa uhai wake aliishi na mume kwa miaka miwili Kijiji cha Songambele na hawakujaaliwa kupata mtoto.

“Tukio la yeye kuonekana akiwa hai mimi nimepigiwa simu nikaenda kushuhudia na kweli nikakuta ni mwenyewe, mwanzo sikuamini ila nilipomuona kwa sura na kuongea naye ndipo niliamini, nilimkuta kwenye ofisi za Mtendaji wa Kata ya Kamalampaka kwa maelezo yao walisema ametokea Mpanda maeneo yasiyojulikana,”anasimulia shemeji wa mwanamke huyo.

Leonard Nkomo ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Kamsisi amesema taarifa hizo alizipata akiwa kwenye kikao cha Mkuu wa wilaya, ambapo anasema katika kikao hicho Mkuu wa wilaya alizungumza kuwa kuna mtu amepatikana baada ya kupotea kwa muda wa miaka mitano.

“Tukaanza kuulizana huyo mtu alikua amepotea au alienda wapi ndio wakasema kuwa alikua amefariki dunia ameonekana kijiji cha Kamalampaka, nilivyofika kijijini ikabidi nimpigie afande mmoja anaitwa Omary akasema niko eneo lako nimemleta huyu mtu alikua amefariki dunia basi nikamwambia ngoja nije nijiridhishe kama ni mwananchi wangu nimuone na mimi.

“Ikabidi nitoke nyumbani nije mpaka hapa na nikashuhudia mimi mwenyewe na nikamtafuta Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ilelanda alikofariki, akasema ni kweli kabisa alifariki miaka mitano aliyopita na nguo aliyozikwa nayo ni hii, ikabidi nimtafute mzee mwingine tena mwenyeji wa kitongoji hiki naye akasema ni kweli mtu huyo alifariki,” amesema Mwenyekiti wa huyo wa kijiji.

Amesema tukio hilo halijawahi kutokea na wananchi wamelipokea kwa mshangao mkubwa, huku kila mtu akitaka kumuona mwanamke huyo.

HabariLEO ilizungumza pia na mwanamke huyo, ambaye amdesema anachokumbuka kuna watu walimchukua wengine akiwaona anawakumbuka wengine hawakumbuki walivaa mavazi yenye rangi nyeusi,nyekundu na nyeupe.

Alisema baada ya kumchukua walimpeleka sehemu isiyojulikana na alianza kurudi mwenyewe kutafuta ndugu zake baada ya kuwakimbia watu hao waliomchukua.

“Huko nilikuwa naishi mazingira magumu nilikua nakula vitu ambavyo havieleweki nakula mchanga, sabuni matope mara wanibake wamenitesa sana wamenipiga wakaniumiza ila hawajanifanyisha kazi yeyote ngumu zaidi ya kunitesa kunipiga kunilisha mchanga na vingine vichafu,” amesema mwanamke huyo ambaye pia hutambulika kwa jina la Mwasi.

Diwani wa Kata ya Kamsisi, Leonard Kiyungi alisema tukio hilo ni la kwanza kutokea na yeye kulishuhudia ,ambapo alifika hadi nyumbani kwa marehemu.

5 comments

Comments are closed.