ALPHONCE SIMBU: Avunja mwiko wa miaka 39 bila dhahabu

BAADHI ya vichwa vya habari vya magazeti mbalimbali ya Tanzania tangu mwanzoni mwa wiki vimesomeka hivi; ‘Simbu aweka rekodi mpya kimataifa’, ‘Simbu aleta heshima’, ‘Simbu aweka rekodi kimataifa’, ‘Dk Samia ampongeza Simbu’, ‘Rais Samia atia neno ushindi wa Simbu’, ‘Rais Samia ampongeza Simbu kutwaa medali ya dhahabu’ na ‘Rais Dk Samia ampongeza Simbu’.

Mwanariadha huyo amepata medali ya dhahabu baada ya kumaliza wa kwanza katika Mashindano ya Riadha ya Dunia yanayoendelea jijini Tokyo, Japan Jumatatu asubuhi. Ni ukweli usiofichika kwamba, Alphonce Simbu ameing’arisha Tanzania katika ulimwengu wa riadha.

SOMA: Simbu aiheshimisha Tanzania, Samia ampongeza

Kawaida kurasa za nyuma ndio maalumu kwa ajili ya habari za michezo lakini Simbu alivunja mwiko huo baada ya kushinda medali hiyo na kujikuta ameandikwa kuanzia kurasa za mbele, ambazo mara nyingi ni za kisiasa hadi za nyuma pia.

Imekuwa hivyo baada ya mwanariadha huyo kuiwezesha Tanzania kupata medali ya kwanza ya dhahabu kutoka katika Mashindano hayo ya Riadha ya Dunia. Ni kipindi cha miaka 39 sasa tangu mashindano hayo yalipofanyika kwa mara ya kwanza jijini Helsinki, Finland na mwanariadha wa Tanzania, Christopher Isegwe akimaliza wa pili na kutwaa medali ya fedha.

Tumewahi kupata medali zingine za dhahabu kutoka katika Michezo ya Jumuiya ya Madola miaka ya nyuma, michezo inayoshirikisha nchi zilizowahi kutawaliwa na Muingereza lakini Mashindano ya Dunia hushirikisha nchi zote duniani. Hivyo, mbali na ukubwa ni magumu pia.

Tangu kuanza kwa mashindano hayo, Isegwe aliendelea kuwa Mtanzania pekee aliyewahi kupata medali kutoka katika mashindano, hadi mwaka 2017, Simbu alipopata medali ya shaba. Hadi sasa ni miaka 31 tangu yaanzishwe mwaka 1986 na hii ni medali ya kwanza ya dhahabu kwa Tanzania tangu mashindano hayo yaanzishwe.

Mafanikio ya Simbu hayakuja haraka, yalikuja kwa jitihada zake za muda mrefu baada ya kushiriki mbio za mashindano hayo makubwa pamoja na Olimpiki katika nchi mbalimbali. Amekuwa akishiriki London Marathon, New York Marathon, Boston Marathon akifanya vizuri kila anaposhiriki na kuboresha muda wake binafsi na kujengea uimara zaidi katika mchezo huo wa marathoni.

Sasa Simbu amekuwa mwanariadha pekee wa Tanzania aliyetwaa medali ya dhahabu kutoka mashindano ya riadha ya dunia tangu mwaka 1989, ikiwa ni miaka 38 tangu Isengwe alipotwaa medali ya fedha. Baada ya ushindi huo, Simbu alisema kuwa pongezi zimuendee mkuu wa majeshi kwa kuwapa muda zaidi wa kufanya mazoezi yaliyomwezesha kufanya vizuri katika mshindano.

Pia, alisema wakati umefika wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) kuelekeza nguvu kwa watoto wadogo na vijana, badala ya kuelekeza nguvu zao zaidi kwake na mwanariadha mwenzake wa mbio ndefu, Gabriel Geay. Amesema hivyo baada ya kuona muda unapotea kwao, kwani umri unakwenda na wakistaafu hakuna wa kuchukua nafasi yao, hivyo ni bora kuwafunza watoto na vijana mchezo huo.

Naye Rais wa RT, Rogath John amesema mbali na kuwaendeleza watoto na vijana, atahakisha michezo ya mbio fupi na mingine, mbali na marathoni inawekewa umuhimu zaidi, tofauti na sasa ambapo marathoni ndio kipaumbele kwa kila mtu.

Amesema ushindi huo ni ishara ya kuondoa mkosi wa kutofanya vizuri katika mashindano mbalimbali ya kimataifa na wataendelea kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali kwa kuwaandaa vizuri wachezaji.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button