Amani iendelee kutawala kampeni Uchaguzi Mkuu

LEO ni siku ya tisa tangu kampeni za uchaguzi zizinduliwe Agosti 28.

Wagombea wa vyama mbalimbali vinavyoshiriki wanaendelea kuchanja mbuga wakishawishi wananchi kwa kuwapa sera zao ili wawapigie kura katika nafasi za udiwani, ubunge na urais.

Katika siku tisa tangu kampeni za Uchaguzi Mkuu zizinduliwe, hali ya amani na utulivu imeendelea kutawala.

Hii ni ishara thabiti kwamba wadau wa kisiasa na wananchi kwa ujumla wanathamini amani kama msingi wa  maendeleo na ustawi wa nchi.

SOMA: Kumekucha kampeni za Uchaguzi Mkuu

Kampeni zimeendelea kila pembe ya nchi kwa njia za amani, zikihamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi bila hofu ya migogoro au vurugu.

Tunawapongeza Watanzania wote sambamba na mamlaka za usimamizi zikiongozwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa kuweka misingi na mazingira yenye kufanikisha mchakato huu kwenda kwa amani.

Hii ni fursa muhimu kwa kila mshiriki wa siasa kuendelea kuonyesha uzalendo, kueneza sera za vyama na kujenga mazingira mazuri ya uchaguzi wenye nidhamu.

Upo msemo wa Kiswahili: ‘Nyota njema huonekana asubuhi’ ukiwa na maana kuwa mambo mazuri au matokeo mazuri yanajulikana mapema, hasa wakati wa mwanzo wa juhudi au kazi.

Msemo huu unadhihirisha uhalisia wa hali ilivyo katika kipindi cha takribani wiki tangu kampeni zianze kwamba hii ndiyo hali itakatawala hadi hapo mchakato mzima wa uchaguzi utakapohitimishwa.

Ni wazi kuwa amani ni nyota njema ambayo Watanzania kwa ujumla hawahitaji kuoneshwa bali wanajionea kwamba imeonekana mapema.

Amani inatoa fursa kwa wagombea na wananchi kuendelea na kampeni zao kwa njia zinazoimarisha umoja, mshikamano na utulivu bila kuwapo chembe za chuki zinazoweza kuathiri mchakato wa uchaguzi.

Mwenendo huu uimarishwe bila kutoa nafasi kwa yeyote kuleta chokochoko na kuharibu sura njema ya Tanzania ambayo siku zote imekuwa mfano mwema wa utulivu kwa mataifa mengine.

Tunahimiza wadau wote wa uchaguzi hususani vyama vya siasa, viongozi wa dini, mashirika ya kiraia, vyombo vya habari na wananchi kwa ujumla kuendeleza amani hii kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya uchaguzi.

Amani ndiyo msingi wa maendeleo ya nchi kwani ni chachu katika kuvutia wawekezaji, kuendesha shughuli za kiuchumi, na kuendeleza ustawi wa kijamii.

Hivyo basi, tunasisitiza kwamba amani iendelee kutawala katika kipindi hiki cha kampeni kuelekea siku ya uchaguzi Oktoba 29, na baada ya uchaguzi.

Ni jukumu la kila mshiriki wa mchakato huu kuhakikisha kuwa amani inazingatiwa kwa hali na mali huku Watanzania wakiendelea kuwa kitu kimoja.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button