Ambindwile autabiria makubwa uchumi wa ‘salon’

IRINGA: KATIKA ulimwengu unaobadilika kwa kasi, sekta ya ‘salon’ imekuwa si tu tasnia ya urembo, bali pia chanzo muhimu cha ajira, kipato na mchango mkubwa kwa uchumi wa taifa.
Haya yamebainika katika kongamano la watoa huduma wa ‘salon’ lililofanyika Iringa na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali, wakiwemo viongozi wa serikali, taasisi za kifedha na wataalamu wa sheria.
Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Kanda ya Iringa, Wakili Moses Ambindwile alisema sekta ya salon imekua kutoka kutumia vifaa duni hadi kuwa taaluma rasmi inayotolewa katika vyuo kama VETA.
“Huduma hizi si za anasa. Zinahitajika na viongozi, wanamichezo, wafanyabiashara, wanajeshi, wake kwa waume, watoto hadi vijana – wote wanahitaji huduma za salon,” alisema.
Ambindwile, ambaye pia amechaguliwa kuwa mwanasheria wa Umoja wa WanaSalon.
Sekta hii inahusisha huduma kama kusuka na kunyoa nywele, kucha, kupaka vipodozi, na huduma za ngozi.
Alisema thamani ya tasnia hii inaendelea kukua kutokana na ukweli kuwa inahusiana moja kwa moja na muonekano wa watu, ambao ni hitaji la msingi kijamii na kitaaluma.
Alisema ikiungwa mkono ipasavyo, sekta hii inaweza kuchangia kikamilifu pato la mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla. Ili kufanikisha hilo, kuna haja ya kuwa na sera maalum za kutambua rasmi sekta hiyo, kuboresha mazingira ya biashara, kutoa elimu ya kisheria na kifedha, pamoja na kuwapa fursa watoa huduma wa salon kushiriki kikamilifu katika ajenda za kitaifa ikiwemo uchaguzi mkuu.
Ambindwile alisisitiza kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 22, inatoa haki ya kufanya kazi kwa Watanzania wote, hivyo hata watoa huduma za salon wana haki hiyo kama ajira rasmi.
Aliwataka washiriki wa kongamano hilo kuhakikisha wanaendesha biashara zao kwa misingi ya sheria ikiwa ni pamoja na kuwa na mikataba rasmi ya kazi na kujiunga na mifumo ya hifadhi ya jamii.
Katika mazungumzo hayo, wakili Ambindwile aligusia pia haki ya watoa huduma wa salon kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu ujao.
“Kama sehemu ya jamii, nanyi mna haki ya kupiga kura na kuchagua viongozi watakaowatetea na kuwatambua. Hii ndiyo njia ya kushiriki katika maamuzi yanayogusa maisha yenu ya kila siku,” alisema.
Katibu wa Chama cha Salon Iringa, Kombo Muzungu, alibainisha changamoto kuu kuwa ni mitaji midogo, ukosefu wa maeneo rasmi ya biashara, na kutotambulika kama sekta rasmi licha ya kuajiri vijana wengi.
“Tunaomba halmashauri zetu ziendelee kututambua, kutupatia maeneo ya kufanyia kazi na kutupatia fursa katika mikakati ya kiuchumi,” alisema.
Oscar Kitise, mmoja wa wanachama, alibainisha kuwa kupitia kongamano hilo wamepata elimu kutoka taasisi mbalimbali zikiwemo NHIF, TRA, na CRDB.
Taasisi hizi ziliahidi kuendelea kushirikiana na watoa huduma za salon katika utoaji wa elimu na mikopo ya masharti nafuu.
Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Rebecca Sanga, aliwahamasisha watoa huduma wa salon kujiamini na kujibrand kama wataalamu wa kweli.
“Ukiweza kujielewa na kujiendesha kisasa, unaweza kupata fedha nyingi kila siku. Wapo wajasiriamali wa salon wanaopata faida ya zaidi ya milioni 25 kwa mwaka,” alisema.
Alitoa wito kwa vijana kutumia fursa zilizopo, hususani mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya halmashauri, na vyuo vya VETA vinavyotoa mafunzo kwa ufadhili wa serikali.