Amchoma mikono mtoto kisa kadokoa chainizi

JESHI la Polisi mkoani Mwanza linamshikilia, Maneno Thomas (35) mkazi wa Chamagati, wilayani Sengerema kwa tuhuma za kumchoma mikono mtoto wake kwa maji ya moto baada ya kumtuhumu kudokoa mboga ya majani aina ya chainizi.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa Mwanza, Wilbroad Mtafungwa, ameeleza kuwa mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo Julai 30, 2023, baada ya kutoka katika shughuli zake.

Mtafungwa ameeleza kuwa mtuhumiwa alipofika nyumbani kwake alimwambia binti yake aitwaye Prisca Maneno (11), apike chakula cha usiku ndipo alipoelezwa kuwa hakuna mboga, kwani ililiwa na mdogo wake Daniel Maneno (9), ambaye anasoma darasa la pili Shule ya Msingi Mtakuja.

“Maneno Thomas alishatengana na mkewe kutokana na vitendo vyake vya kipigo cha mara kwa mara na mwanamke aliamua kuondoka,” amesema Mtafungwa.

Amesema mtuhumiwa aliwasha moto kisha kuchemsha maji yalipochemka, alimuita mwanae Daniel Maneno na kumwagia maji hayo katika mikono yake yote miwili na kumsababishia maumivu makali.

Baada ya kufanya tukio hilo mtuhumiwa aliamua kumfungia mtoto huyo chumbani kwake na wananchi wa eneo hilo walishtuka kutomuona mtoto Daniel siku mbili mfululizo, ndipo walipoanza kufatilia na kugundua amefanyiwa ukatili huo.

 

Habari Zifananazo

Back to top button