anzania, UAE kukuza ushirikiano uchumi, biashara

TANZANIA na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) zimekubaliana kuendeleza uhusiano wa kiuchumi na kibiashara. Makubaliano hayo yamefanywa na Rais Samia Suluhu Hassan alipozungumza na Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu na Mtawala wa Dubai, Sheikh Mohammed bin Rashid Al Maktoum.

Viongozi hao walizungumza pembezoni mwa Mkutano wa Dunia wa Serikali (WGS 2026) mjini Dubai juzi. Rais Samia na Al Maktoum wamekubaliana kukamilisha mikataba ya ushirikiano wa biashara na mikataba ya uwekezaji wa nchi na nchi ili kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji baina ya Tanzania na UAE Viongozi hao pia walijadili utekelezaji wa miradi ya pamoja na uwezekano wa kuanzishwa kwa safari mpya za anga kwa Shirika la Ndege la Emirates ikiwemo safari ya Kilimanjaro – Zanzibar kukuza utalii na biashara.

Sheikh Maktoum aliahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa karibu kupitia miradi ya maendeleo kwa manufaa ya ustawi wa uchumi wa pande zote mbili. Uhusiano wa kibiashara kati ya Tanzania na UAE umeendelea kuimarika kwa kasi na thamani ya biashara imeongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 985.31 mwaka 2018 hadi Dola za Marekani bilioni 2.1 mwaka 2024 na kuiwezesha Tanzania kuwa mshirika wa nne kwa ukubwa wa biashara wa UAE barani Afrika.

Ushirikiano huo umechangia kukua kwa masoko ya bidhaa za Tanzania, kuimarika kwa viwanda na sekta ya usafirishaji, utalii na huduma za usafiri wa anga, hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa. Wakati huo huo Rais Samia alisema Tanzania imejipanga kuwa kitovu cha biashara na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Amesema hayo aliposhiriki katika mjadala wa kimataifa kuhusu uwekezaji kwenye mkutano wa Jukwaa la Serikali Duniani juzi. Rais Samia alisema itafanya hivyo kwa kuunganisha mtandao wake na nchi jirani kupitia bandari, reli na barabara, hivyo kurahisisha usafirishaji wa bidhaa, madini na nishati. SOMA: Rais Samia kuanza ziara China

Amesisitiza umuhimu wa uthabiti wa sera, uwazi wa mifumo ya utawala na ulinzi wa maslahi ya wawekezaji, kama msingi wa kujenga imani ya muda mrefu kwa wawekezaji wa ndani na wa kimataifa. Rais Samia ameainisha mchango wa sekta ya utalii katika uchumi wa Taifa, akiitaja kuwa ni moja ya sekta zinazoongoza kwa kuingiza fedha za kigeni, sambamba na sekta nyingine za madini, nishati na kilimo.

Ameeleza pia namna Tanzania inavyoshirikiana na taasisi za fedha za kimataifa na kikanda ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Benki ya Dunia katika kufadhili miradi mikubwa ya maendeleo. Rais Samia amesisitiza serikali inaendelea kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi kupitia ubia wa kimkakati (PPP) ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button