Apendekeza adhabu za kimila zifutwe, ni kubwa kuliko makosa

BAADHI ya wakazi wa Wilaya ya Butiama mkoani hapa wameiomba serikali kupiga marufuku mila kandamizi, zinazotoa adhabu kali kwa wanaotenda makosa mbalimbali.

Walimwambia Mkuu wa Wilaya hiyo, Moses Kaegele juzi wakati wa kufanya usafi katika Kituo cha Afya cha Butuguri.

Walisema wazee wengine huanzisha migogoro ndani ya vijiji ili baadhi ya wananchi waonekane wametenda makosa na kupewa adhabu hasa ya kutoa faini ya kiasi kikubwa cha pesa.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mmoja wa wananchi, Aneth Joshua, alipendekeza adhabu za kimila zifutwe na badala yake makosa yote yawe yanafikishwa katika vyombo vya sheria ili haki itendeke.

“Hata kosa dogo mtu anapigiwa yowe kukusanya wanakijiji, ambao wakati mwingine hujichukulia sheria mkononi bila kujua ukubwa wa kosa husika,” alisema.

Alisistiza kwamba adhabu hizo zinawarudisha nyuma kimaendeleo, kwani wazee wa kimila wanatoza pia faini ya idadi kubwa ya mifugo.

Mkuu wa Wilaya alikiri kupokea malalamiko ya aina hiyo kila wakati, akawataka wazee wa kimila kubadilisha utaratibu kwani adhabu zinasadikika kutoendana na ukubwa wa makosa yanayotendeka.

Kadhalika adhabu hizo zinakiuka sheria za nchi, akawataka kutoa taarifa ya makosa yote polisi.

“Na vikundi vya ulinzi shirikishi pia vihusishwe ,vitafikisha taarifa panapohusika, kwa utatuzi wa haraka wa changamoto yoyote katika jamii,” alisema na kuongeza:

“Hata ofisi za watendaji wa kata zinaweza kutatua baadhi ya migogoro, akawataka wazee hao wa kimila na jamii kwa ujumla kuzitumia kwani kila mmoja anatakiwa kufuata sheria”.

Mmoja wa wazee wa Kijiji cha Butuguri, Mgini Mwisendi, alisema kutoza faini watu wanaokiuka mila na desturi ni suala lililopo enzi na enzi katika kulinda maadili na si kwa kumuonea mtu.

Alisema wazee wa kimila wataitana kufuatilia suala la watu kuonewa na kulipatia ufumbuzi wa haraka, kama lipo.

Habari Zifananazo

Back to top button