Arthritis: Ugonjwa unaoweza kusababisha ulemavu

DAR ES SALAAM: Wataalamu wa afya wameonya kuhusu arthritis, kundi la magonjwa zaidi ya 100 yanayoweza kushambulia viungo vya mwili na kusababisha ulemavu ikiwa hayatagunduliwa na kutibiwa mapema.
Arthritis si ugonjwa mmoja, bali ni jina linalotumika kuelezea magonjwa mbalimbali yanayoathiri viungo na wakati mwingine sehemu nyingine za mwili.

Profesa Francis Furia, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), na Daktari Bingwa wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, amesema arthritis inaweza kumpata mtu wa umri wowote, wakiwemo watoto na wazee, na huathiri wanawake na wanaume.

Hata hivyo, amesema baadhi ya aina za arthritis huwapata zaidi watu wenye umri mkubwa, huku wanawake wakiwa katika hatari zaidi ya kupata baadhi ya magonjwa hayo.

Ameeleza kuwa Arthritis ni miongoni mwa sababu kubwa za ulemavu duniani, lakini Tanzania bado ina tafiti chache zinazoonyesha ukubwa halisi wa tatizo hilo nchini.

“Utafiti uliofanyika katika Hospitali ya KCMC kwa wagonjwa waliolazwa katika wodi za magonjwa ya ndani kati ya mwaka 2017 na 2019, ulibaini wagonjwa 129 kati ya 8,023 walikuwa na arthritis. Kati ya wagonjwa hao, 71, sawa na asilimia 55, walikuwa na umri wa zaidi ya miaka 60,” amesema Prof Furia.

Amefafanua kuwa dalili zilizobainika zaidi zilikuwa maumivu ya viungo kwa wagonjwa 69, kuvimba viungo kwa wagonjwa 38 na kukakamaa kwa viungo kwa wagonjwa 18.

“Utafiti mwingine uliofanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa watu waliopatiwa huduma kati ya mwaka 2012 na 2019, ulibaini watu 52 wenye matatizo ya arthritis. Baadhi ya wagonjwa hao walikuwa na ulemavu uliowafanya washindwe kwenda shule,” ameeleza.

DALILI

Kwa mujibu wa Profesa Furia, dalili za arthritis zinaweza kutofautiana kulingana na aina ya ugonjwa, lakini zinazojitokeza mara nyingi ni maumivu, kukakamaa na kuvimba kwa viungo.

Viungo vinavyoweza kuathirika ni pamoja na vya mikono, miguu na mgongo.
Amesema watu wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusu arthritis, hali ambayo inaweza kuchelewesha utambuzi wa ugonjwa na kuongeza hatari ya mtu kupata ulemavu wa muda mrefu.

Amesema hata baadhi ya wataalamu wa afya bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu aina mbalimbali za magonjwa yanayosababisha arthritis.

MATIBABU YANAPATIKANA

Profesa Furia amesema watu wenye dalili za arthritis wanaweza kupata huduma nchini, kwani hospitali zina uwezo wa kufanya vipimo muhimu vya utambuzi na kutoa dawa.

Amesema hospitali za rufaa nchini pia zina kliniki maalumu kwa ajili ya wagonjwa wenye arthritis.

Kauli hiyo imetolewa wakati Tanzania ikiadhimisha kwa mara ya kwanza Siku ya Arthritis Duniani, inayofanyika kila mwaka tarehe 12 Oktoba.

Siku hiyo iliasisiwa mwaka 1996 kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu arthritis, kuwahamasisha watu kutafuta matibabu mapema na kupunguza ulemavu unaoweza kusababishwa na magonjwa hayo.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Achieve Your Dreams”, inayotafsiriwa kama “Timiza Ndoto Zako.”

MATIBABU TANZANIA

Licha ya changamoto hizo, Profesa Furia amesema wagonjwa nchini hawalazimiki kusafiri nje ya nchi kutafuta huduma za arthritis, kwa kuwa matibabu yanapatikana ndani ya Tanzania.

Amesema hospitali nchini zina uwezo wa kufanya vipimo muhimu kwa ajili ya kutambua ugonjwa huo na wagonjwa wanaweza kupata dawa zinazohitajika.
“Hospitali za rufaa pia zina kliniki maalumu zinazowahudumia wagonjwa wenye arthritis” ameongeza.

WANASEMA NINI WENYE ARTHRITIS 

Kwa upande wake, Salum Kigembe, mmoja wa wagonjwa wa arthritis amewashauri wenye ugonjwa huo, kuwasikiliza wataalamu wa afya, na kuzingatia dawa sahihi.

“Mimi nadhni jambo la muhimu kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya, na kuwa na usahihi wa matumizi ya dawa,” amesema Kigembe.

Naye, Rahma Omari, mazazi wa mtoto, Hudheifa Haji wenye arthritis amefafanua kuwa mtoto wake alianza kuumwa mwaka 2016, ila uligundulika 2017 ambapo lilianza joto kwenye mwili wa mtoto huyo.

Amesema kila aina ya dawa waliyompa ilishindwa kushusha joto, hata hivyo walijaribu pia kutumia dawa za maumivu ila baada ya joto kupotea yakaja maumivu.
“Nilikuja Muhimbili alifanya vipimo mbalimbali na baadaye 2018 wakagundua ana arthritis akaanza kutumia dawa hadi sasa ana miaka 10 anaendelea kutumia dawa,” amesema Rahma.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button