Asas ahimiza vijana kujiandikisha uchaguzi mitaa

KATIKA juhudi za kuhakikisha ushiriki wa wananchi katika uchaguzi wa serikali za mitaa, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Salim Asas amehimiza wakazi wote wa Mkoa wa Iringa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwa ajili ya uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, mwaka huu.

Akizungumza na wanahabari mara baada ya kujiandikisha katika kituo cha Chuo cha Afya kata ya Gangilonga mjini Iringa, Asas amesisitiza umuhimu wa serikali za mitaa katika maendeleo ya jamii na kutolea wito wananchi kushiriki kikamilifu ili kuchagua viongozi watakaosukuma maendeleo ya kweli.

Kiongozi huyo alibainisha kuwa, kupitia serikali za mitaa, wananchi wanapata fursa ya kuchagua viongozi wa karibu zaidi nao, ambao watakuwa na jukumu la kuongoza shughuli mbalimbali za maendeleo ya kijamii, kama vile kuboresha miundombinu, afya, elimu, na huduma nyingine za msingi.

Advertisement

Asas alisema, “Viongozi wa serikali za mitaa wanachangia sana katika kuhakikisha huduma muhimu zinawafikia wananchi. Wananchi wote wanapaswa kuelewa kuwa hii ni nafasi ya kuwachagua wale wenye uwezo wa kubadilisha hali zetu na kuleta maendeleo kwa vitendo.”

Pia aliongeza kuwa zoezi la kujiandikisha ni la muhimu sana kwani linawapa wananchi haki ya kikatiba ya kushiriki katika uchaguzi na akaonya kuwa kutokujiandikisha ni sawa na kukosa sauti katika uongozi wa eneo husika.

SOMA: Asasi: Vijana wamtete Rais

Alitoa wito maalum kwa vijana, akisema kuwa wao ndio chachu ya maendeleo na wanapaswa kutumia fursa hii kujiandikisha kwa wingi na baadaye kushiriki katika uchaguzi huo.

Akifanya ukaguzi katika baadhi ya vituo vya kujiandikisha, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Kheri James amesema; “Kila mmoja wetu anapaswa kujiandikisha ili tupate nafasi ya kuwachagua viongozi wanaostahili kutuletea maendeleo.”

James amesema zoezi la uandikishaji linaendelea katika vituo mbalimbali ambapo wananchi wanaweza kufika na kujisajili kwa muda mfupi na kuendelea na shughuli zao.

SOMA: Asasi: Uongozi usiwe fursa kiuchumi

Aliwata viongozi wa ngazi zote kuendelea kuhamasisha wananchi ili kufanikisha zoezi hilo kwa kiwango kikubwa.