Asas atoa Sh Milioni 151 kujenga ofisi za CCM Kilolo

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama cha Mapinduzi, Salim Asas ametumia Sh Milioni 151 kati ya Sh Milioni 179.6 kukamilisha ujenzi wa ofisi ya chama hicho ya wilaya ya Kilolo.

Kukamilika kwa ofisi hiyo iliyozinduliwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Mizengo Pinda kumeelezwa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kilolo, John Kiteve kwamba kumekamilisha ndoto yao ya kuwatoa katika jengo chakavu walilokuwa wakilitumia kama ofisi yao.

Pamoja na ujenzi wa ofisi hiyo, Asas ametoa ahadi ya kujenga ofisi zake zitakazokuwa za kisasa katika kata zote 106 za mkoa huo wakati  wa maadhimisho ya sherehe za miaka 46 ya chama hicho yaliyofanyika kimkoa wilayani Kilolo.

Ahadi za ujenzi wa ofisi hizo zitakazojengwa ndani ya miaka mitano ijayo kwa gharama ya kati ya Sh Milioni 20 na Sh milioni 50 imekuja huku akiwa tayari amejenga ofisi ya kisasa ya chama hicho katika kata ya Kiyowela wilayani Mufindi iliyogharimu zaidi ya Sh Milioni 51.

“Baada ya kuzindua ofisi hii ya wilaya, nikuahidi Mheshimiwa Pinda kwamba tutaendelea kukuita mkoani kwetu kuzindua ofisi tutakazojenga katika kata zote za mkoa wa Iringa, kazi nitakayofanya kwa kushirikiana na wanachama na viongozi wenzangu. Kwa hiyo usichoke,” Asas alisema.

 

Wanachama wa chama hicho kupitia Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Rukia Mkindu walisema watapanga kufanya maombi maalumu kumuombea Mnec huyo, ili Mwenyezi Mungu ampe maisha marefu zaidi na zaidi.

“Misaada yake haihesabaki katika chama hiki. Amesaidia sana huku nyuma, anatoa sasa na anaahidi kuendelea kukisaidia chama chake na wananchi wa Iringa kwa ujumla. Kiongozi huyu anahitaji maombi maalumu,” alisema Mkindu.

Akizungumza na wapenzi na wanachama wa chama hicho baada ya uzinduzi wa ofisi hiyo, Pinda ambaye pia ni Waziri Mkuu Mstaafu alimpongeza Asas kwa juhudi zake za kukifanya chama hicho kifanye kazi kisasa na katika mazingira bora.

Aidha Pinda alizungumzia umoja na mshikamano katika chama hicho akikitaka kisiwapuuze viongozi wake waliomaliza muda wao wa uongozi.

“Uongozi ni kupokezana vijiti, waliondoka madarakani tusiwapuuze; tuwaheshimu na tuwatumie, hao sio maadui wa chama ni sehemu yetu,” alisema.

Habari Zifananazo

Back to top button