Asas azima mvutano machinga, halmashauri Iringa

Asas azima mvutano machinga, halmashauri Iringa

HEKIMA, busara na huruma za Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Salim Asas zimegeuka kuwa tiba kwa machinga waliokuwa na hasira baada ya jeshi la Polisi kuwatimua kwa mabomu katika eneo la ndani la makaburi ya Mlandege mjini Iringa walilovamia ili kufanyia biashara zao.

Machinga hao wanaotakiwa kufanya biashara zao nje ya makaburi hayo, walitawanywa kwa mabomu jana jioni baada ya kukaidi amri ya serikali iliyowataka wote walioingia ndani ya eneo la makaburi kutoka mara moja.

Pamoja na kufanya ukaidi huo, machinga hao waliziba kwa mawe moja ya barabara zilizopo jirani na eneo hilo kama moja ya mkakati wao wa kupinga kuondolewa katika eneo la ndani la makaburi na kuzua taharuki kwa watumiaji wengine wa barabara hiyo.

Advertisement

Katika kikao cha maelekezo kilichoitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego ndani ya Uwanja wa Samora mjini Iringa, Asas aliwashawishi machinga hao kufanya biashara zao nje ya makaburi hayo kama ilivyoelekezwa na mamlaka zingine.

“Ni nani kati yetu hii leo anaweza kuwa tayari kuona kaburi la ndugu yake linatumika kufanyia biashara?…kama ambavyo nyinyi hamuwezi kukubali na wengine ni hivyo hivyo. Kwahiyo naomba muelewe, serikali ina nia njema na ninyi na wenye makaburi haya,” alisema.

Katika kuwasaidia machinga hao kuboresha biashara na mazingira yao ya kufanyia biashara katika eneo la nje ya makaburi hayo, Asas alitangaza kuchangia Sh Milioni 100.

“Kati ya fedha hizo Sh Milioni 50 zitatumika kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya kufanyia biashara zenu ikiwa ni pamoja na kuezeka na Sh Milioni 50 nyingine kwa ajili ya mfuko wenu wa kuweka na kukopa,” alisema na kuibua shangwe nderemo na vifijo toka kwa machinga hao.

“Kuhusu miundombinu matarajio yangu ni kuona meza za biashara kwa ajili ya akina mama na vijana zinajengwa kwa mpangilio mzuri na kugaiwa kwa walengwa,” alisema na kuibua shangwe zaidi.

Asas alitoa mchango huo baada ya halmashauri ya manispaa ya Iringa kuahidi kutenga Sh Milioni 150 kwa ajili ya chama cha kuweka na kukopa cha machinga hao wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 1,000.

Akifafanua kuhusu fedha hizo, Meya wa Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada alisema; “Fedha hizo tumezitoa ili kuwawezesha machinga kukuza mitaji yao.”

Alisema halmashauri yake ina nia njema na machinga na katika mikakati yake ya sasa na ya muda mrefu ni pamoja na kuhakikisha wanakuwa na maeneo salama ya kufanyia biashara yasio na migogoro.

Machinga hao ambao awali walikuwa wakifanyia biashara zao mbele ya wafanyabiashara wa maduka katika eneo maarufu la mashine tatu na maeneo mengine katikati ya mji wa Iringa, walihamishiwa nje ya makaburi ya Mlandege baada ya kulalamikiwa na wenye biashara za maduka.

Mwenyekiti wa machinga hao, Yahaya Mpelembwe alimshukuru Asas akisema fedha alizotoa tayari zimeanza kufanya kazi ya kuboresha eneo la nje ya makaburi hayo.

“Kwa utaratibu huu eneo la nje linaweza kutosheleza idadi kubwa ya machinga kwa sababu meza zinajengwa vipimo maalumu na mipaka sio holela holela,” alisema na kuzungumzia nguvu ya fedha inavyoweza kuhamisha mlima na kuzima migogoro.

Alisema Mkuu wa Mkoa wamekuwa naye toka saa 12.00 asubuhi ya leo ili kuhakikisha shughuli hiyo ya ujenzi inafanyika kwa kuzingatia maslahi ya machinga wengi.

Baada ya hekaheka ya jana, Mkuu wa Mkoa aliwashukuru machinga hao kwa kuwa waungwana na kukubaliana na maelekezo ya serikali yaliyowataka watoke ndani ya eneo la makaburi.

“Waliolazwa pale ni ndugu zetu, majirani zetu na marafiki zetu, tunapaswa kuwakumbuka kwa kuwapa heshima yao. Sio ubinadamu kufanya biashara juu ya makaburi yao. Niwashukuru sana kwa kuilewa serikali,” alisema.