Asas: Wanachama CCM shirikini kikamilifu kura za maoni

IRINGA: Mjumbe wa Kamati Kuu (MCC) ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Salim Abri Asas, ametoa wito kwa wanachama wa chama hicho kote nchini kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika zoezi la kura za maoni, akisema ni njia pekee ya kupata viongozi bora watakaosimamia ipasavyo Ilani.
Akizungumza baada ya kushiriki kura hizo katika kata yake ya Gangilonga, mjini Iringa Asas amesema mchakato huo, unaoendelea nchi nzima kufuatia marekebisho ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977, ni fursa ya kidemokrasia ambayo kila mwanachama anapaswa kuitumia kwa maslahi ya maendeleo ya taifa.
“Kupiga kura ni haki na wajibu wa kila mwanachama. Ni kupitia hatua hii ndipo tunapowachagua viongozi watakaotekeleza Ilani yenye malengo ya kutatua changamoto za wananchi wetu,” alisema Asas.

Aidha, aliipongeza CCM chini ya uongozi wa Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kusimamia mchakato mzima kwa umakini, uwazi na utulivu, akisema hatua hiyo inaonyesha dhamira ya kweli ya chama katika kukuza misingi ya demokrasia ya ndani.
SOMA ZAIDI
Asas amesisitiza kuwa wanachama wanaposhiriki kikamilifu, wanakuwa sehemu ya kuamua mustakabali wa maendeleo ya taifa, na kwamba ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha viongozi watakaochaguliwa wanakuwa na uwezo, uadilifu na maono ya kweli ya kuwatumikia wananchi.


