Je, Ahmed Asas atavunja ukimya ubunge Iringa Mjini?

IRINGA: Joto la kisiasa limepanda Iringa Mjini huku macho na masikio ya wananchi yakielekezwa kwa mfanyabiashara maarufu na mdau wa maendeleo ya jamii, Ahmed Asas.

Ahmed jina lake linatajwa kwa sauti kubwa miongoni mwa wana-CCM na wananchi wanaomshinikiza ajitokeze kuwania ubunge katika uchaguzi mkuu ujao.

Kesho, Juni 28, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinafungua rasmi dirisha la kuchukua fomu kwa makada wake wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, ikiwa ni hatua muhimu kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba.

Wakati hamasa ikizidi kushika kasi, wakazi wa Iringa Mjini wanaendelea kuulizana: Je, Ahmed Asas atatinga katika ulingo wa siasa mwaka huu?

Tayari kumekuwepo na mjadala mpana miongoni mwa wanachama wa CCM na wananchi wa kawaida kuhusu uwezekano wa mfanyabiashara huyo kijana na mdau maarufu wa shughuli za kijamii kujitokeza kuwania ubunge kupitia tiketi ya chama hicho tawala.

Ahmed, ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kusaidia makundi mbalimbali ya kijamii kwa muda mrefu, anatajwa kuwa mmoja wa watu wanaopewa nafasi kubwa na wananchi kutokana na moyo wake wa kusaidia, ukaribu wake na jamii, pamoja na mchango wake katika kuinua wajasiriamali wadogo, hususan vijana na wanawake.

Katika mahojiano na baadhi ya wakazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, wengi walieleza matumaini yao kuwa Ahmed ataitikia wito wa wananchi kwa kujitokeza kuchukua fomu ya kuwania ubunge.

“Kwa kweli kama ni Ahmed Asas atagombea, mimi binafsi sitasita kumpigia kura. Ni mtu anayefaa kuwa mwakilishi wetu bungeni. Ana moyo wa kusaidia na amekuwa bega kwa bega na sisi wajasiriamali wadogo,” alisema John Mkini, mfanyabiashara ndogondogo kutoka eneo la Ipogolo.

Kwa upande wake, Mwajuma Kulanga, mama wa nyumbani kutoka Isakalilo, alisema Ahamed amekuwa msaada mkubwa kwa vijana katika eneo hilo, hasa kwenye masuala ya uwezeshaji na maendeleo ya vikundi vya kijamii.

“Ni kijana mwenye maono na anayegusa maisha ya watu moja kwa moja. Kama atagombea, naamini ataungwa mkono na wengi,” alisema Mwajuma.

Kesho, makada wa CCM wenye nia ya kuwania nafasi za uongozi katika maeneo mbalimbali nchini wanatarajiwa kuanza kuchukua fomu, hatua itakayoweka wazi sura halisi ya mbio za uchaguzi mkuu wa mwaka huu ndani ya chama hicho.

Wakati vuguvugu la kisiasa likizidi kupamba moto, macho na masikio ya wakazi wa Iringa Mjini sasa yameelekezwa kwa Ahmed Asas – kusubiri kuona kama ataamua kujitosa rasmi katika kinyang’anyiro cha kuwania ubunge.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button