WADAU wa asasi zisizokuwa za kiserikali zinazohusika na masuala ya afya wamesema wanatamani kuona wahudumu wa afya ya jamii wanapata utambulisho ili waweze kushughulikia mambo mengi katika ngazi ya jamii.
Utambulisho huo ni kuwa na nyaraka zinazowatambua na posho ya kila mwezi kwa maana wao ndio hutambua na kuanza kujua shida katika ngazi za chini.
Hayo yalisemwa mwishoni kwa wiki wakati wa mkutano ulioandaliwa na Shirika la People’s Health Movement Tanzania (PHM) na kushirikisha waandishi wa habari na asasi sizizo za kiserikali mkoani Dodoma.
Ofisa Habari na Mahusiano wa Shirika la Alliance on Traditional Practices and Women Empowerment (ATPWE), Mihwela Mapembe alisema wahudumu wa afya ngazi ya jamii wamekuwa na mchango mkubwa hasa maeneo ya vijijini ni vyema likafanyika jambo kwa ajili yao.
“Tunatamani wapate utambulisho ili wawe na vitambulisho na posho ya kila mwezi kwa maana wao ndio hutambua na kuanza kushughulikia mambo mengi katika ngazi ya jamii,” alisema.
Alisema wamekuwa wakiwatumia kufanya uelimishaji hasa katika kupinga ukeketaji ambao kwa sasa umekuja kwa njia mpya ya bibi wanawafinya au kuwasugua na dawa sehemu za siri za watoto wachanga.
Mkurugenzi Mtendaji wa PHM, Godfrey Philemon alisema lengo la mkutano huo ni kukutana na waandishi wa habari na asasi za kiraia zinazofanya kazi kwenye eneo la afya ya jamii kisha wataenda kukutana na watoa huduma na wauguzi wa afya ngazi ya jamii.
“Malawi wana siku ya kitaifa kwa ajili ya kutambua mchango wa wahudumu wa afya ya jamii na nchi nyingine zinawalipa,” alisema.
Aliiomba serikali kuweka mikakati ya kuboresha maslahi ya wahudumu hao kwani wamekuwa wakifika maeneo ambayo watu wengine hawafiki.
Kwa upande wake Ofisa Uelimishaji na uhusiano kutoka PHM, Thomas Edward alisema kuwa shirika hilo limesajiliwa kama asasi isiyokuwa ya kiserikali, linafanya kazi kuhakikisha huduma za afya kuwa haki kwa Watanzania wote.
“Kuangalia mijadala ya kusera, kuunga mkono jitihada za serikali katika kupaza sauti kwa watu wa kawaida,” alisema.
Alisema kuwa kazi yao kubwa ni uelimishaji, utetezi ili kila mtu apate huduma ya afya katika kiwango kizuri.
Mratibu wa mtandao wa Asasi za kiraia Mkoa wa Dodoma (NGONEDO), Edward Mbogo alisema huduma bora za afya ni suala la msingi kwa kila binadamu.