DAR ES SALAAM; TAASISI ya Tiba na Mifupa Muhimbili (MOI) imesema wagonjwa 405 sawa na asilimia 5.2 wameongezeka kutoka 7,797 mwaka 2023 hadi wagonjwa 8,202 Desemba mwaka jana ambapo asilimia 59 ni wa ajali za barabarani.
Hayo yalibainishwa jana na Kaimu Meneja wa Kitengo cha Utafiti, Elimu na Ushauri MOI, Joshua Ngahyoma alipozungumza na HabariLEO na kuongeza kuwa wagonjwa hao wanatokana na matatizo mbalimbali, zikiwemo ajali za barabarani.
Ngahyoma alisema miongoni mwa wagonjwa hao, wagonjwa 3,350 ambao ni sawa na asilimia 41 wametokana na aina zingine za ajali, ikiwemo kuanguka huku wagonjwa 4,852 sawa na asilimia 59 wakitokana na ajali za barabarani.
“Januari hadi Desemba (2024) tumepokea wagonjwa 8,202 katika kitengo cha dharura, kati ya hao majeruhi wa ajali barabarani ni 4,852 sawa na asilimia 59, kati yao asilimia 21 ni ajali za magari na asilimia 38 ni ajali za bodaboda,” alisema.
Akifafanua kuhusu wagonjwa waliotokana na ajali za barabarani, Ngahyoma alisema majeruhi 3,105 walitokana na ajali za bodaboda na majeruhi 1,747 walitokana na ajali za magari.
“Majeruhi 1,397 sawa na asilimia 45 ni madereva bodaboda, majeruhi 963 sawa na asilimia 31 ni abiria wa bodaboda na majeruhi 745 sawa na asilimia 24 ya majeruhi waliosababishwa na bodaboda waliokuwa watembea kwa miguu,” alisema.
Akizungumzia huduma ambazo wamepatiwa wagonjwa hao baada ya kufikishwa MOI, Ngahyoma alisema baadhi ya wagonjwa ambao wamepata majeraha madogomadogo ambayo hayakuhitaji upasuaji walihudumiwa katika kitengo cha dharura.
“Wagonjwa ambao wamepata majeraha madogomadogo ambayo hayakuhitaji upasuaji walikuwa 2,957 sawa na asilimia 36 ya wagonjwa wote waliohudumiwa katika kitengo cha dharura,” alisema.
“Waliopata majeraha makubwa walikuwa 5,245 sawa na asilimia 64 ya wagonjwa wote waliohudumiwa katika kitengo cha dharura, wagonjwa 2,610 sawa na asilimia 50 walifanyiwa upasuaji wa dharura ndani ya saa 24 na wagonjwa 427 sawa na asilimia nane walipata huduma ya uangalizi wa karibu katika vyumba vya wagonjwa mahututi,” aliongeza.
Alisema wagonjwa hao wote ambao wamefikishwa MOI wamepata majeraha ya kuumia vichwa, migongo, kuvunjika mifupa mirefu, kukatika miguu, kuvunjika nyonga pamoja na vidonda vikubwa ambavyo vinasababishwa na ajali hizo.