Asilimia 60 madini ujenzi Dar yanazalishwa Pwani
DODOMA; Asilimia 60 ya madini ujenzi yanayotumika kwenye ujenzi wa miradi ya kimkakati katika Mkoa wa Dar es Salaam huo yanazalishwa kutokea Mkoa wa Pwani.
Naibu Waziri wa Madini, Dk Stephen Kiruswa ametoa kauli hiyo bungeni leo Septemba 6, 2023 alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mariam Kisango aliyetaka kujua Mkoa wa Dar es Salaam umenufaika vipi na uzalishaji wa madini ujenzi yaliyozalishwa katika mkoa huo.
“Pamoja na kwamba Mkoa wa Dar es Salaam unazalisha na unanufaika na madini ujenzi, hata hivyo wastani wa asilimia 60 ya madini ujenzi yanayotumika kwenye ujenzi wa miradi ya kimkakati katika Mkoa huo yanazalishwa kutokea Mkoa wa Pwani katika Wilaya za Mkuranga, Bagamoyo, Kisarawe na Kibaha.
“Mheshimiwa Spika, madini ujenzi yanayozalishwa katika Mkoa wa Dar es Salaam yanajumuisha mchanga, kifusi na limestone; ambayo yanazalishwa katika Wilaya za Kigamboni, Ilala na Kinondoni.
“Kwa mwaka wa fedha 2022/23, makusanyo ya mrabaha na ada ya ukaguzi yatokanayo na madini hayo katika Mkoa wa Dar es Salaam yalifikia kiasi cha shilingi billioni 1.9,” amesema Naibu Waziri.
Amesema Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini itaendelea kuimarisha usimamizi katika uzalishaji wa madini ujenzi katika Mkoa wa Dar es Salaam na nchini kote kwa ujumla, ili kuongeza manufaa ya madini hayo kwa wananchi mmoja mmoja na Taifa.