Asilimia 60 watuhumiwa rushwa ya ngono ni vyuoni

DSM; TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni imesema kuwa asilimia 60 ya waliokamatwa wakituhumiwa rushwa ya ngono ni wahadhiri wa vyuo vikuu na vyuo vya kati.

Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam, Mchunguzi Mkuu na Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kinondoni, Bibie Msumi katika kikao cha majadiliano kilichoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) kwa kushirikiana na Mfuko wa Udhamini wa Wanawake Tanzania (WFT-T) kupitia mradi wa kuangazia rushwa ya ngono kwa wanahabari wanawake.

Amesema utafiti wa mwaka 2020 waliofanya Takukuru ulibaini kuwepo rushwa ngono katika taasisi za elimu ya juu, huku watu wengi waliokamatwa kwa makosa hayo ya rushwa ya ngono ni wahadhiri wa vyuo vikuu na vya kati.

“Asilimia 60 tuliowakamata kwa makosa ya ngono ni wahadhiri wa vyuo vikuu na vya kati, baadhi yao hukumu zimeshatolewa na wengine kesi zinaendelea mahakamani,” amesema.

Anasema kwa mujibu wa Kifungu cha 25 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11/ 2007, mtu yeyote ambaye kwa kutumia nafasi yake au mamlaka yake katika kutekeleza majukumu yake anaomba au kutoa upendeleo wa kingono au upendeleo mwingine wowote kama kigezo cha kutoa haki mfano kumfaulisha kimasomo, kumpa ajira, kupandishwa cheo, kutoa haki au upendeleo wowote unaotambulika kisheria, atakuwa ametenda kosa chini ya kifungu hiki.

Habari Zifananazo

Back to top button