Asilimia 94 wana hatari kuambukizwa malaria

WAZIRI wa Afya ,Ummy Mwalimu amesema licha ya kupungua kwa vifo na maambukiza ya malaria nchini, bado asilimia 94 ya Watanzania wako hatarini kupata ugonjwa huo.

Akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Malaria Duniani yaliyofanyika leo  jijini Dar es Salaam, Waziri Ummy amesema maambukizi ya malaria yamepungua kutoka asilimia 18.4 mwaka 2015 hadi asilimia 8.1 mwaka 2022, lakini bado wanashuhudia vifo na Watanzania wakipata ugonjwa wa malaria.

“Ugonjwa wa malaria maana yake watu hawaendi kazini, hawaendi shambani ,viwandani  watu hawafanyi uzalishaji na watoto wetu wanaweza kupoteza hata siku tano hata saba za kuwepo shuleni kwa hiyo malaria bado ni tishio,”amesisitiza.

Amesema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau wanatekeleza mpango wa miaka mitano wa kutokomeza malaria, ambapo wamejikita katika mambo manne, ambayo ni udhibiti wa mbu wanaoeneza malaria, uchunguzi , tiba, kinga na ufuatiliaji na tathamini ya mwendo wa malaria.

“Kubwa tumegawa nchi katika matabaka manne,  tumeangalia kiwango cha maambukizi ya malaria na tumeweza kupunguza mikoa yenye kiwango kikubwa cha malaria chini ya asilimia moja kutoka sita hadi tisa, hiyo inafanya vizuri,” amesema.

Ametaja mikoa inayofanya vizuri kuwa chini ya asilimia moja ni Dar es Salaam, Songwe, Manyara, Arusha , Kilimanjaro, Iringa, Singida , Njombe, na Mwanza ambayo pia wanataka ifikie asilimia sifuri.

Ummy amesema wanaendelea kununua na kusambaza dawa na vitendanishi katika vituo  vya afya na pia wanafanya ufuatiliaji wa ubora, usalama na ufanisi wa dawa za malaria na wamejiridhisha kuwa asilimia 96 dawa zina uwezo wa kutibu.

“Kwa kushirikiana na wadau tunaendelea kutoa elimu changamoto tuliyonayo ni usugu wa mbu dhidi ya dawa aina Pareto ambayo hutumika katika vyandarua vya dawa mpaka sasa zaidi ya asilimia 70 wamejenga usungu dhidi ya dawa hiyo, “ amesema.

Amebainisha kuwa ili kutatua changamoto hiyo wizara imesambaza vyandarua  vipya vyenye viambata vinavyofaa na wataendelea kukabiliana na usugu wa dawa hizo, lakini pia wanaangalia namna ya kupata vyandarua vya kisasa.

“Changamoto ya pili ni uhaba wa rasilimali fedha kutekeleza mfano afua ya kunyunyiza viuadudu kwenye mazalia ya mbu na kunyunyizia dawa katika kuta na tuna halmashauri 61 ambazo zimepata afua hiyo, sasa tunafanya katika halmashauri sita za Kasulu, Kibaondo , Biharamulo, Kakonko, Bukombe na Ukerewe DC .

Habari Zifananazo

Back to top button