Askari atuhumiwa kumuua kijana kwa risasi

ASKARI Polisi wa Kituo kidogo cha Magereza kilichopo Kisongo jijini Arusha, anadaiwa kumuua kwa kumpiga risasi tatu mkazi wa Kata ya Olasiti, Oloresho Sindio wakati kijana huyo akijaribu kumsihi askari kuwaachia mifugo yake iliyokuwa imekamatwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo alikiri kuwapo kwa tukio hilo na kueleza kuwa polisi wanaendelea na uchunguzi wakati mwili wa marehemu ukiwa umehifadhiwa katika Hopitali ya Mount Meru kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Akizungumza jana jijini Arusha, Diwani wa Kata ya Olasiti, Alex Martin alisema tukio hilo ni la juzi saa 7:00 mchana, maeneo ya Kiwanja cha Ndege Kisongo jijini hapa na kijana huyo alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mount Meru. Alimtaja askari anayetuhumiwa kwa jina moja la Eliwaha.

Alisema alipata taarifa juu ya tukio hilo na kufika eneo la tukio, lakini alikuta damu nyingi zikiwa zimetapakaa na matundu ya risasi kwenye barabara ya lami na kijana huyo hakuwepo.

“Nilipofika eneo la tukio nilizungumza na mashuhuda wakiwemo vijana wawili waliokamatiwa mifugo yao, ambao walinieleza kuwa mara ya kwanza askari huyo alimpiga marehemu risasi pajani na kuanguka chini na kisha alimsogelea na kumpiga risasi nyingine mbili akiwa chini na baadaye alimburuza na kumpakia kwenye gari la polisi alilokuja nayo na kuondoka naye,” alieleza.

Alisema baada ya maelezo ya mashuhuda hao, aliamua kwenda katika Hospitali ya Mkoa Mount Meru na kumkuta kijana huyo akiwa na hali mbaya lakini baadaye usiku alifariki dunia kutokana na kuvuja damu nyingi.

Akielezea tukio hilo lilivyoanza, alidai askari huyo alifika eneo la tukio baada ya kupata taarifa kwamba kuna mifugo imeingia kwenye eneo lisiloruhusiwa kwa ajili ya malisho.

Alisema askari huyo alikamata mifugo hiyo na wachungaji wawili na kuanza kuipeleka kusikojulikana, lakini ghafla alitokea Olasio (marehemu) akiwa na pikipiki na alipowaona vijana hao  aliwatambua na kuamua kwenda kuzungumza na askari huyo ili kujua kilichotokea na kumsihi askari huyo awaachie na mifugo yao.

“Lakini askari huyo alionekana kuwa mkali ndipo marehemu alipoamua kuondoka na kwenda kuchukua pikipiki yake ili aendelee na safari yake, lakini kabla hajafika mbali askari huyo alichomoa silaha yake na kumpiga risasi moja kwenye mguu na kijana kuanguka chini, baadaye alimsogelea na kumfyatulia risasi nyingine mbili eneo la mapajani,” alisema.

Alisema askari huyo aliamua kumburuza  majeruhi huyo hadi alipokuwa ameacha gari na kumpakia na kuondoka naye na baadaye kumpeleka katika Hospitali ya Rufaa Mount Meru, lakini usiku alipoteza maisha akiwa anapatiwa matibabu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika Hosptali ya Rufaa ya Mkoa ya Mt Meru, baba mdogo wa marehemu, Richard Mollel, alisema mtoto wao alipigwa risasi na askari huyo saa 7:00 mchana na baada ya kufika eneo la tukio alikuta mwili ulishachukuliwa na kukimbizwa.

“Baada ya kufika Mount Meru tulimkuta  mtoto wetu akiwa na hali mbaya, ambapo baada ya muda mfupi alihamishiwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) katika hospitali hiyo,” alisema.

Kwa mujibu wa Mollel, walijulishwa na madaktari kuwa inahitajika damu kwa ajili ya kumuongezea.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella alipohojiwa juu ya tukio hilo alithibitisha kuwa na taarifa hizo na kusema kuwa anafuatilia na atatoa ufafanuzi baadaye.

Habari Zifananazo

2 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button