Askari zaidi wakamatwa  usafirishaji mirungi

WATU watatu wakiwemo askari wawili wameingizwa katika sakata la Mrakibu Msaidizi wa Polisi wa Kituo cha Polisi wilayani Arumeru mkoani Arusha, John Shauri la kusafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi magunia manne yenye kilo 264.

Shauri alikamatwa Julai 16, mwaka huu jijini Arusha baada ya Julai 14, mwaka huu kuwakimbia Polisi wa Kizuizi cha Minjingu mkoani Manyara pale alipotakiwa kusimama na kupekuliwa na baadaye kulitekeleza gari aina ya Noah Vox yenye namba za usajili 264 CUS likiwa limebeba mirungi hiyo.

Akizungumza na HabariLEO jana, Kaimu Kamanda wa Polisi Manyara, Lucas Mwakatundu alisema hadi sasa wamekamatwa watu wanne katika tukio hilo akiwemo raia na uchunguzi wa tukio bado unaendelea.

Advertisement

Mwakatundu alikataa kutaja majina ya watuhumiwa hao watatu kutokana na uchunguzi kuendelea ikiwemo kusaka watu wengine wanaodaiwa kuhusika na biashara hiyo.

Shauri anadaiwa alikuwa akifanya biashara hiyo haramu ya kusafirisha mirungi akiwa na sare za jeshi la polisi ili iwe njia rahisi yeye kupita katika vizuizi mbalimbali vya polisi Makuyuni, Minjingu na Babati.