Askofu afariki baada ya kuhubiri ibada ya mazishi

George Chiteto

KANISA la Anglikana Tanzania limepata pigo la kuondokewa na Askofu wake wa Dayosisi ya Mpwapwa, George Chiteto muda mfupi baada ya kiongozi huyo kutoa mahubiri katika misa ya kuaga mwili wa mke wa Askofu wa Dayosisi ya Nyanda za Juu Kusini, Julius Lugendo, Hilda.

Katika ibada hiyo iliyofanyika kwenye  Kanisa la Mfalme Kristo la Madaba,  Muheza mkoani Tanga, wakati akihubiri, Askofu Chiteto alisema kifo cha Hilda ni kizuri kwa kuwa alifikwa na mauti akiwa amelala. Alisema na yeye alitamani afe kifo hicho na aone mwanga.

Miongoni mwa waliokuwapo katika ibada hiyo, akiwamo mwanahabari wa kituo cha habari cha Kanisa Anglikana Dayosisi ya Tanga, Maiko Luoga alisema askofu alipomaliza mahubiri, alidondoka na kuishiwa nguvu wakati ibada ikiendelea.

Advertisement

Akihubiri, Askofu Chiteto alisema: “…nikasema kifo changu kiwe hivi hivi, isibadilike hata sentensi moja, yaani unapokuja kuniita (Mungu) mlango uwe  umefunguliwa, sio fungueni, wenye hadhi hapa ni wachache.

“Je, baba zangu sisi watumishi wakubwa, kwenye haya makanzu mazuri, lakini je, wenye hadhi sio wachache, wote tuna hadhi au wengine wataambiwa sorry sorry sikujui, mimi hunijui mimi, sikujui unapotoka…mimi nilikuwa pale mzee wa kanisa, unaambiwa wewe huku hakuna wazee wa kanisa kuu wala wapi, tunataka wenye hadhi hapa.”

Alisema Yesu anarudisha hadhi katika bustani na kuwataka waumini wajitahidi kuingia sasa maana mlango uko wazi. Aliongeza: “Hii dunia ina mwenyewe na mlango una mwenyewe mmoja tu, atakaposimama na kuufunga na kama ulichelewa hukurudishiwa hadhi yako utakuwa umechelewa too late to catch the bus.”

Askofu Chiteto alisisitiza: “Dada Hilda atukumbushe kwamba ingia sasa, mlango bado umefunguliwa, lakini lazima uwe na hadhi kubwa.”

Katika taarifa ya Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Maimbo Mndolwa alisema baada ya mahubiri, dakika chache baadaye aliishiwa nguvu na kupoteza fahamu kabla ya kukimbizwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Muheza alikofikwa na mauti.

Agosti 28, 2022, Chiteto aliwekwa wakfu kuwa askofu wa tatu wa Dayosisi ya Mpwapwa.