Askofu ahimiza kodi, tozo kwa maendeleo

WATANZANIA wametakiwa kuipenda nchi kwa moyo wa dhati kwa kujenga utashi na utayari wa kulipa kodi na tozo za serikali ili kujenga taifa imara lenye maendeleo kwa wote sambamba na kuheshimu mamlaka zilizopo.

Rai hiyo ilitolewa na Askofu wa Kanisa la Maombezi (GRC), Anthony Lusekelo alipozungumza na vyombo vya habari, Dar es Salaam jana kuzungumzia uhusiano wa kodi na Ukristo.

Lusekelo alisema hakuna taifa liliwahi kuendelea bila kulipa kodi na hiyo imewekwa wazi katika Biblia tangu wakati wa torati Mungu alipounda taifa la Israeli na kuwatengea viongozi alioona wanafaa kuliongoza.

“Katika Biblia, Mungu zamani za torati alijiundia taifa lake, mpango wa kuunda taifa lake ulianza alipomuita Ibrahim kutoka katika nchi ya kwao kwenda katika nchi atakayomwonesha. Mungu alitengeneza mifumo ya kifedha kwa taifa hilo la Israel akatoa na mwongozo wa kuongoza taifa hilo ikiwa ni pamoja na adhabu kwa watakaovunja sheria,” alisema.

Alifafanua kuwa kodi na tozo zinazozungumzwa sasa hazina tofauti na zaka na dhabihu zilizokuwa zikitolewa na Wayahudi wakati huo na hata waliposhindwa kulipa walihesabiwa kuwa ni wezi waliobeba laana.

“Wakati huo ukishindwa kutoa sadaka unaitwa mwizi, ukishindwa kutoa zaka na dhabihu unabeba laana. Hutafanikiwa uingiapo wala utokapo,” alisema.

Aliendelea kusema kuwa wakiwa na viongozi waliochaguliwa na Mungu miaka 40 baada ya kuundwa taifa la Israel, Wayahudi walikataa kuongozwa na Waamuzi, wakataka kuchagua viongozi wao.

Alisema walimpata kiongozi wa kwanza aliyeitwa Sauli kwa mchakato uliosimamiwa na Samweli ambaye alitamka kuanza kwa mfumo wa kutozwa kodi ili taifa hilo liendelee na ndipo kwa mara ya kwanza neno kodi lilitamkwa.

Alisema hata wakati huo, Wayahudi walipinga mpango wa kulipa kodi hivyo suala la kodi halijawahi kukosa migogoro tangu wakati huo hata sasa hivyo jambo la muhimu ni utayari wa Watanzania kulipa kodi na tozo za serikali kwa maendeleo ya nchi bila kujali viwango.

Kuhusu mtazamo wa kuwakamua maskini, Lusekelo alisema kodi na tozo zote hukatwa kulingana na kipato na kiwango cha fedha kinachohusika katika miamala inayofanywa hivyo hakuna mtu takayekatwa tozo au kulipa kodi isiyoendana na uwezo wake.

Askofu huyo aliwataka Watanzania kuheshimu viongozi, akisisitiza wawape ushirikiano kwa kile alichosema wamechaguliwa wao watoe mawazo na ubunifu wao katika kusukuma gurudumu la maendeleo ya nchi.

Habari Zifananazo

Back to top button