Ataka sheria kubana wanaume kliniki

Ataka sheria kubana wanaume kliniki

MKUU wa Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Julius Mtatiro ameiagiza halmashauri ya wilaya hiyo kukamilisha haraka mchakato wa kutunga sheria ndogo itakayobana wanaume wenye tabia ya kuwachelewesha wake zao wajawazito kufika katika vituo vya afya kwa wakati.

Mtatiro alisema hayo jana wakati akizindua wiki ya chanjo kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano na wasichana wenye umri wa miaka 14 katika zahanati ya Mapambazuko inayomilikiwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Tunduru-Masasi.

Alisema serikali kupitia Wizara ya Afya imeweka utaratibu wa mama anapohisi mjamzito kuwahi kliniki mapema wakati wote wa ujauzito na hata baada ya kujifungua ili kuangalia maendeleo ya afya zao na kuongeza kuwa chanjo inasaidia kuwakinga wajawazito na hatari ya kupata magonjwa na kwa watoto wanaozaliwa kuwa na kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali yanayozuilika ikiwemo surua, kupooza, kifua kikuu na kifaduro.

Advertisement

 

Mkuu wa wilaya ya Tunduru,Julius Mtatiro akimpa matone ya kukinga magonjwa mbalimbali mtoto wa wiki sita Vaileth Shungwe,aliyekaa mama wa mtoto,Luiza Ndunguru.

Mtatiro alisema kuna watu wanapotosha ukweli kuhusiana na umuhimu wa chanjo ikiwemo chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana wenye umri wa miaka 14 walioko shuleni na nyumbani kwa kueleza kuwa, ina madhara jambo ambalo halina ukweli.

“Chanjo hii ni muhimu sana kwa ajili ya watoto wetu waliopo shule na wale walioko nyumbani, nawaomba wazazi hasa akina mama msikubali kuwasikiliza wapotoshaji, changamkieni chanjo ili kuwaokoa watoto wenu na hatari ya kupata ugonjwa huo,” alisema.

Mtatiro aliwataka wanawake kuhakikisha wanakula chakula chenye virutubisho vyote muhimu ili kujenga familia zenye afya bora, badala ya kula chakula cha aina moja kila siku ambacho kinaweza kusababisha tatizo la udumavu na utapiamlo kwa watoto wao.

Baadhi ya akina mama waliohudhuria uzinduzi wa wiki ya chanjo katika wilaya ya Tunduru,wakimsikiliza Mkuu wa wilaya hiyo Wakili Julius Mtatiro(hayupo pichani) jana kabla ya uzinduzi rasmi wa zoezi la chanjo.

Katika hatua nyingine, Mtatiro aliwakumbusha wananchi juu ya kutunza na kujiwekea akiba ya chakula wanachozalisha kwa ajili ya matumizi ya familia zao na kuepuka tabia ya kuuza chakula chote kutokana na tamaa ya kupata fedha.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *