Ataka wimbo wa Makongoro kampeni ya watoto

IRINGA;  MKUU wa Mkoa wa Iringa Halima Dendego, ametaka wimbo wa marehemu Mzee Makongoro uliopigwa redioni kwa miaka mingi kuhamasisha ulaji wa vyakula vyenye lishe bora kutumika kuhamasisha utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Makuzi, Malezi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ( PJT-MMMAM).

Wimbo huo ‘kuleni kuku, mayai, mboga samaki maziwa..’ ulitamba sana Redio Tanzania miaka ya 80 na 90 na kwa mujibu wa Dendego ulisaidia sana kuwahamasisha Watanzania kula vyakula mchanganyiko kwa lishe endelevu.

Akizindua utekelezaji wa programu hiyo mkoani mwake ili kama ilivyo maeneo mengine nchini ichochee afua za mtoto mwenye miaka chini ya nane kufikia ukuaji timilifu, Dendego alisema haelewi kwa nini vyombo vya habari hususani redio zinazoendelea kuongezeka nchini hazipigi tena wimbo huo.

Alisema afya ya mtoto ni sehemu muhimu ya mpango wa maendeleo ya mtoto kwa hiyo ni muhimu kuhakikisha anapata lishe bora, chanjo, huduma za afya, na anaishi katika mazingira salama katika kukuza maendeleo yake.

“Mpango wa maendeleo ya mtoto ili kufikia ukuaji timilifu unapaswa kuzingatia afya yake kama kipengele muhimu cha kujenga msingi wa maisha yake ya baadaye,” alisema.

Akisisitiza umuhimu wa wimbo huo katika kuelimisha jamii umuhimu wa malezi na makuzi ya awali ya mtoto kwa kuzingatia lishe bora, Dendego aliziagiza wilaya na halmashauri zake zote katika kila mkutano kuhakikisha unapigwa sambamba na utoaji wa elimu ya utekelezaji wa programu hiyo.

Aidha Mkuu wa Mkoa huyo alizungumzia kile alichokiita malezi ya kijinga  kwa watoto yanayohusisha baadhi ya wazazi na walezi kuruhusu watoto wao kutumia simu za mkononi wakiwa na umri mdogo jambo linaloathiri makuzi na maadili yao.

“Kwa kuwapa watoto wenu simu wakiwa na umri mdogo mnataka wapate nini kutoka katika simu hizo, mnajua matokeo yake?” Alihoji na kuongeza kwamba matumizi ya simu za mkononi kwa watoto yanasababisha wakutane na maudhui yasifaa yanayochangia kuharibu mienendo yao.

Dendego alisema ukuaji wa watoto zaidi ya milioni 250 waliopo kusini mwa Jangwa la Sahara, ambalo Tanzania ni sehemu yake ni muhimu sana kwa kuzingatia kwamba kanda hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi za kijamii, kiuchumi, umasikini, lishe bora na magonjwa na kuwekeza katika watoto wa eneo hilo kunaweza kuleta matokeo mazuri.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Veronica Kessy alisema, ukuaji wa mtoto unapaswa kuchukuliwa kwa umakini mkubwa kwa kuzingatia lishe bora, huduma za afya, elimu, upendo, na usalama.

“Kila hatua ya ukuaji wa mtoto ina umuhimu wake, kuanzia ujauzito mpaka utu uzima. Kutoa upendo, kuwajibika kama mzazi, na kuhakikisha mazingira salama ni muhimu kwa maendeleo mazuri ya mtoto wako,” alisema.

Alizungumzia pia ukatili wa watoto akiitaka jamii ya Iringa kuendelea kupaza sauti dhidi ya vitendo hivyo na wanaobainika kufanya makosa hayo wasiwe na msamaha mbele ya sheria.

Habari Zifananazo

2 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button