ATCL yarejesha Safari za ndege Iringa

HATIMAYE, Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) limeanza tena safari zake kati ya Dar es Salaam na Iringa baada ya kusitisha huduma hiyo kwa miaka minane, hatua itakayochochea ukuaji wa uchumi na sekta ya utalii mkoani Iringa.

Safari hizo mpya, zinazofanyika mara tatu kwa wiki, zinatoa fursa kwa wasafiri kufika Iringa ndani ya dakika 60 pekee, tofauti na safari za barabara zinazochukua saa nane au zaidi.

Leo, ndege ya ATCL yenye uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 70 ilitua Iringa ikiwa imejaa, kabla ya kurejea Dar es Salaam ikiwa imejaa pia.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika katika Uwanja wa Ndege wa Iringa, Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Mhandisi Peter Ulanga, alisema kurejeshwa kwa safari hizi ni hatua muhimu kwa maendeleo ya mkoa huo.

“Huduma hii si tu kwamba inarahisisha usafiri, bali pia inasaidia kukuza biashara, utalii, na maendeleo ya kiuchumi kwa ujumla. Kwa sasa, abiria wanaweza kusafiri kutoka Dar es Salaam hadi Iringa na kurudi kwa gharama nafuu ya Sh 199,000 pekee,” alisema Mhandisi Ulanga.

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, aliipongeza ATCL kwa hatua hiyo na kueleza kuwa serikali inazidi kuwekeza katika sekta ya usafiri wa anga ili kuhakikisha mikoa yote inakuwa na huduma bora za usafiri.

“Kurejeshwa kwa safari hizi kunatoa nafasi kwa wafanyabiashara, wawekezaji, na watalii kufanikisha shughuli zao kwa ufanisi zaidi. Tunaendelea kuboresha miundombinu ya viwanja vya ndege nchini ili kuongeza idadi ya safari za anga,” alisema Profesa Mbarawa.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba, alibainisha kuwa huduma hiyo itachochea maendeleo ya sekta ya utalii, ikizingatiwa kuwa Iringa ni lango kuu la utalii kusini na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, mojawapo ya hifadhi kubwa na maarufu Afrika.

“Kwa sasa, watalii na wawekezaji wanaweza kufika Iringa kwa urahisi zaidi, jambo linaloashiria fursa mpya za biashara na ukuaji wa uchumi wa mkoa huu,” alisema Serukamba.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Kheri James alisema safari hizi zitasaidia kuongeza idadi ya wageni na kuchochea uwekezaji mpya katika hoteli, huduma za utalii, na biashara nyingine zinazotegemea wageni kutoka nje ya mkoa.

Mmoja wa abiria kutoka Norway, Osmond Ueland alisema kurejesha safari hizi, Tanzania inathibitisha dhamira yake ya kuimarisha sekta ya usafiri wa anga na kuhakikisha kila mkoa unapata fursa ya maendeleo kupitia huduma za haraka na za uhakika.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button