SHAHIDI wa kwanza katika kesi ya mauaji inayomkabili Hemed Ali, ameieleza mahakama jinsi mshtakiwa huyo alivyoishi ndani ya nyumba yake na baadaye kupokea taarifa kuwa kuna mtu alifukiwa katika nyumba hiyo na mshtakiwa.
Shahidi huyo, Hamjat Nassoro ambaye ni mmiliki wa nyumba aliyokuwa akiishi mshtakiwa maeneo ya Ilala Sharif Shamba mkoani Dar es Salaam, alieleza hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Joyce Minde.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Grace Lwila, Hamjat alidai kuwa Hemedi alianza kuishi katika nyumba hiyo Julai 23, 2013 kwa mkataba wa mwaka mmoja ambao uliisha Julai 23, 2014.
“Awamu ya kwanza tulikuwa na mkataba, awamu ya pili alinilipa kodi bila mkataba lakini hakumaliza muda alikaa miezi mitano akasema anahama amenunua nyumba Magomeni,” alisema shahidi huyo.
Aliendelea kudai akiwa ndani ya nyumba hiyo mshtakiwa alitoa malalamiko kuwa kuna tatizo la shimo la maji taka kujaa mara kwa mara, hivyo aliomba amruhusu aende kwa mjumbe akaombe kuchimba shimo nje ya nyumba ili atapishe maji taka naye akamruhusu.
Alidai hata hivyo mjumbe hakutoa ruhusa hiyo na Ali alirudi kwa Hamjat akimwomba amruhusu achimbe shimo kwa ndani ya uzio wa nyumba.
“Aliponiomba nikamruhusu lakini nilimwambia achimbe kama ana hakika atafukia vizuri kama palivyokuwa, alichimba katika eneo la dirisha la mbele, baada ya hapo sikufuatilia tena kilichoendelea kwa sababu mimi nikishampangisha mtu huwa sitaki kumbughudhi,” alidai.
Alidai baada ya miezi mitano ya awamu ya pili akiwa safarini mshtakiwa alihama bila kumwambia na aliporejea ndipo alipompa taarifa kwamba amehama na akamtuma mtu apeleke ufunguo kwake.
Akielezea tukio la kuzikwa mwili kwenye nyumba hiyo, Hamjat alidai Februari 9, 2015 alipokea simu kutoka kwa polisi wakimtaka aende katika nyumba yake kuna tukio mshtakiwa alilifanya naye akaenda.
“Nilipofika niliwakuta polisi na watu wa afya kutoka Hospitali ya Amana, waliniambia kuna mwili umezikwa na wanataka kufukua niliwaruhusu. Niliondoka eneo hilo kwa kuwa sikuwa najisikia vizuri kushuhudia tukio hilo hivyo sikushuhudia mwili ukitolewa mahali hapo,” alisema.
Kabla ya ushahidi kuanza mshtakiwa huyo alisomewa mashtaka yake ambapo ilidaiwa Juni 12, 2014 alimuua ,Farahani Abdulsalum, mashtaka ambayo aliyakana mbele ya Hakimu Minde. Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa leo.