MWENYEKITI mpya wa Umoja wa Afrika (AU) Rais wa Angola, João Lourenço ameelezea umuhimu wa kuendelea na umoja huo akisisitiza kushughulikia changamoto zinazolikabili bara, ikiwemo migogoro na mabadiliko ya tabianchi.
Lourenço alisema hayo mjini Addis Ababa, Ethiopia jana kwenye mkutano wa kawaida wa 38 ulioanza jana, unaotarajiwa kumalizika leo.
“Dhamira yangu ni kushughulikia changamoto zinazolikabili bara hili, kama vile migogoro, maendeleo ya kiuchumi, na mabadiliko ya tabianchi na vipaumbele vingine,” alisema.
Lourenço amechukua kiti hicho jana akichukua nafasi ya Rais Mohamed Ould Cheikh AI- Ghazouani wa Jamhuri ya Kiislam ya Mauritania.
Mkutano huo unatoa fursa muhimu kwa viongozi wa Afrika kutafakari kuhusu bara hilo, kushughulikia masuala ya dharura na kuthibitisha tena dhamira yao ya umoja.
Kwa upande wa mwenyekiti anayemaliza muda wake wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC), Moussa Faki Mahamat alisisitiza umuhimu mkubwa wa umoja wa Afrika kuzingatia changamoto za kimataifa zinazozidi kuongezeka.
Faki alikumbuka mafanikio ya kipindi chake cha uongozi, akitambua changamoto kubwa zinazoikabili Afrika katika miaka ya karibuni.
“Lazima Afrika iendelee kupambana na shinikizo la kimataifa na migogoro ya kikanda, ni kushikana na kuwa wamoja tu ndio bara letu litapata mustakabali bora,” alisema.
Aliwaomba viongozi wa Afrika waendelee kuwa makini katika dira ya pamoja ya amani, maendeleo, na mshikamano.
Alisema uamuzi utakaofanywa kwenye mkutano huo utaifanya Afrika kuwa imara. Alisisitiza viongozi wa bara hilo kuwa imara na wamoja.
Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), António Guterres, alionya kuwa mzozo wa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), unaweza kusababisha vita ya kikanda.
“Raia wanateseka kutokana na mwendelezo wa ghasia za kikatili, mapigano yanayoendelea huko Kivu Kusini kutokana na kusonga mbele kwa M23, yanatishia kulitumbukiza eneo lote kwenye janga,” alisema.
Katika mkutano huo, ulifanyika uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kamisheni ya AUC akichukua nafasi ya Faki na Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti, Mahamoud Ali Youssouf alishinda kwa kura 33 akimbwaga mpinzani wake, gwiji wa siasa wa Kenya, Raila Odinga aliyejitoa raundi ya sita.
Katika uchaguzi huo ambao pia Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Madagascar, Richard Randriamandrato alishiriki, ilimlazimu, Youssouf kusubiri mpaka raundi ya sita ambayo aliibuka na ushindi.
Raundi ya kwanza, Odinga aliongoza kwa kupata kura 20, Youssouf 18, Randriamandra kura 10, raundi ya pili Odinga aliongoza tena kwa kura 22, Youssouf kura 19 na Randriamandrato kura saba.
Raundi ya tatu Youssouf aliongoza kwa kura 23, Odinga 20 na Randriamandra alipata kura tano.
Raundi ya nne Youssouf alipata kura 25 na Odinga 21, raundi ya tano Youssouf alipata kura 26 na Odinga 21 na raundi ya sita Youssouf alpata kura 26 na Odinga 22.
Wakati huo huo, mkutano huo pia ulitarajiwa kujadili kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia iliyopendekezwa na Tanzania kupitia kwa Rais Samia Suluhu Hassan anayeshiriki mkutano huo pia.
Rais Samia ni kinara wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi Afrika na kwa Tanzania mwaka jana alizindua kampeni ya miaka 10 kuhakikisha mpaka mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.
Mkutano huo pia utajadili taarifa ya ushiriki wa Umoja wa Afrika kwenye mkutano wa nchi tajiri duniani (G20), utekelezaji wa Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika na taarifa kuhusu masuala ya mabadiliko ya tabianchi.