Auawa kwa kukutwa na aliyekuwa mke wa mtu

Jeshi la Polisi Mkoani Geita linamshikilia Athumani Baseka (39), fundi seremala na mkazi wa kijiji cha Kamhanga wilayani Geita kwa tuhuma za mauaji ya Faida Lucas (34) ambaye ni mkulima na mkazi wa kijiji cha Bugalama.

Tukio hilo lilitokea usiku wa Oktoba 30 majira ya saa sita usiku katika kitongoji cha Mwamushiki kijiji na kata ya Bugarama wilaya na mkoa wa Geita ambapo marehemu alikutwa na mwanamke aliyewahi kuwa mke wa mtu.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Safia Jongo amethibitisha na kuwaeleza waandishi wa habari kuwa kiini cha tukio hilo ni wivu wa kimapenzi.

Advertisement

Kamanda amesema marehemu aliuawa kikatili kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali kichwani, utosini na sehemu za mashavu na kupelekea kutokwa na damu nyingi na kupoteza uhai wake.

“Mtuhumiwa na mke waligombana yule mwanamke akaamua kurudi kwao, na wakati akiwa kwao akaanzisha mahusiano mengine na Faida ambaye ni marehemu.

“Ndipo alipowavamia hiyo saa sita usiku na kufanya mauaji hayo, mtuhumiwa amekamatwa, upelelezi ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani”, amesema.

Kamanda amesema jeshi la polisi kupitia polisi jamii linafanya kazi kubwa kuongea na jamii juu ya hatua za kuchukua pale wanapokutana na visa vya usaliti kwenye ndoa (famizi) ili kuepuka kuchukua sheria mkononi.

“Naendelea kutoa rai kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi, kama unahisi kuna mtu ana visasi ni vyema kumpeleka kwenye vyombo vya sheria ili hatua za kisheria zichukuliwe zaidi,” amesema Kamanda.