Aunt Ezekiel: Comfy Mummy itawafanya wanawake wajiamini

DAR-ES-SALAAM : MWIGIZAJI maarufu wa filamu na tamthilia, Aunt Ezekiel, amesema kuwa anafurahi sana kwa ujio wa taulo maalum za Comfy Mummy, akisema kuwa zitamjengea kujiamini na kumuwezesha kuendelea na shughuli zake bila bugudha baada ya kujifungua mtoto wake watatu.

Aunt Ezekiel, ambaye ni balozi wa taulo hizi, alisema juzi jijini Dar es Salaam kuwa katika safari yake ya kujifungua watoto wake wawili wa awali, alikumbana na changamoto kubwa kutokana na vifaa alivyokuwa akivitumia.

“Nimeshajifungua watoto wawili, na ilikuwa ni lazima niandae nguo za ndani na taulo za kutosha kila nilipokuwa naenda hospitali, jambo ambalo lilikuwa linanikera. Taulo zilizokuwa zinapatikana zilijaa haraka, na hivyo kunifanya nisiwe na uhakika, na kujiona kama nimechafuka,” alisema Aunt Ezekiel.

Aliongeza kuwa ujio wa taulo za Comfy Mummy utampa nafasi ya kujihisi huru, kwani taulo hizo zitampa uhakika na kumuwezesha kuwa na amani wakati wa safari yake ya kujifungua. “Taulo hizi zitampa mama uhuru na faraja, na kwa kweli wanawake wanahitaji kuwa na vifaa vya usalama na faraja wakati wa kujifungua,” alisisitiza.

SOMA: Aomba taulo za kike ziondolewe VAT

Mkurugenzi wa Masoko na Mauzo wa Kampuni ya Comfy Mummy, Irene Mville, alisema kuwa anaamini kuwa taulo hizi zitawafaidi wanawake wengi wanaojiandaa kujifungua au waliojifungua.

Alisema kuwa bidhaa hizi zitawasaidia akina mama kujikinga na magonjwa hasa baada ya kujifungua, kipindi ambacho wanawake wengi hupitia mabadiliko ya kimwili, kama vile hedhi ya uzazi.

“Taulo hizi zitawasaidia wanawake kujistiria na kujikinga na magonjwa baada ya kujifungua, kipindi ambacho wanawake wengi wanakutana na changamoto kutokana na hedhi ya uzazi,” alisema Irene.

Balozi wa bidhaa hizo, Zamaradi Mketema, alisema kuwa Comfy Mummy imekuja kama suluhisho muhimu kwa wanawake, akiongeza kuwa miaka ya nyuma wanawake walikumbana na changamoto kubwa kwa kutumia vitambaa na taulo zisizo bora, lakini taulo za Comfy Mummy zinatoa suluhisho la kweli.

“Hii ni bidhaa ya kipekee, na katika nchi zilizoendelea, taulo hizi zilitumika kwa muda mrefu. Ni suluhisho ambalo litasababisha wanawake kufanya shughuli zao bila matatizo,” alisema Zamaradi.

Mkurugenzi wa Afya Check, Isack Maro, alisema kuwa taulo za Comfy Mummy zina faida kubwa, hasa kiafya. Alifafanua kuwa taulo hizi ni salama kwa kuwa zinavaliwa kama nguo za ndani (chupi), na pia mama anaweza kuzivaa na kuendelea na shughuli zake za kila siku.

Alisema kuwa taulo hizi pia zina plastiki maalum inayozuia maji yasipenye na kuathiri via vya uzazi, jambo ambalo litamsaidia mama kuwa na furaha na kupunguza msongo wa mawazo, hali itakayosaidia maziwa kutoka kwa mama kwa ufanisi.

“Taulo hizi zitaongeza furaha kwa mama, na kwa kuwa mama atakuwa salama, atakuwa na hali nzuri, jambo litakalosaidia uzalishaji wa maziwa,” alisema Isack Maro.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button