Yanga waikunia kichwa Mtibwa Sugar

DAR ES SALAAM: KOCHA Msaidizi wa Yanga, Patrick Mabedi, amesema mchezo wao dhidi ya Mtibwa Sugar utakuwa mgumu na kuwataka wachezaji wake kuwa makini ili kuhakikisha wanapata pointi tatu muhimu hapo kesho.
Yanga baada ya kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika wanarejea kwenye ligi na kesho watakutana na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa KMC Complex.
“Kila mchezo una ugumu wake. Kwenye ligi lazima ushindani uwepo na tunaheshimu kila mpinzani. Tunahitaji kuwa makini sana kwenye mchezo wa hapo kesho dhidi ya Mtibwa. Kwa sasa tunachokifanyia kazi mazoezini ni kuhakikisha wachezaji wanatumia vyema kila nafasi wanayoipata,” amesema Mabedi.
Amesema anaamini kikosi cha Yanga kipo katika mwendelezo mzuri wa kiufundi, na kadri muda unavyosonga, timu itazidi kuwa bora zaidi kimbinu.
Akizungumzia hali ya mshambuliaji Prince Dube, Mabedi amesema hana shaka na uwezo wa straika huyo raia wa Zimbabwe, akisisitiza kuwa atarejea kwenye ubora wake.
“Dube amefanya mambo mengi mazuri. Nafahamu ana mzigo mkubwa mabegani mwake, lakini kwa uwezo alionao atakaa sawa. Kuna presha nyuma yake, hiyo ni kawaida kwa wachezaji wakubwa popote pale. Usipofunga lazima maswali yawe mengi, lakini ni suala la muda Dube atarejea kwenye makali yake, sina wasiwasi,” amesema.
-Amewapongeza mashabiki wa Yanga kwa kujitokeza kwa wingi katika mchezo uliopita, akiwataka waendelee kutoa sapoti kwenye mechi zijazo.

Kwa upande wake, mchezaji wa Yanga Offen Chikola, alisema kikosi kimejipanga kurejea kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya kurejea kutoka kwenye mashindano ya kimataifa.
“Tumetokea kwenye mashindano ya kimataifa, tunakutana na mchezo mgumu. Hakuna namna nyingine zaidi ya kupambana kupata pointi tatu. Hatupo kileleni kwenye msimamo hivyo ni lazima tuhakikishe tunarejea juu,” alisema Chikola.



