Aomba taulo za kike ziondolewe VAT

SERIKALI imeombwa kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya asilimia 18 kwenye taulo za kike ili kuwezesha bidhaa hiyo kupatikana kwa bei rahisi na kuwafikia walengwa kwa wakati.
Ombi hilo limetolewa hivi karibuni na Mwanafunzi Mtanzania anayesoma Dubai katika Falme za Kiarabu, Arjun Kaur Mittal kwa Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alipotembelea ofisini kwake.
Arjun amesema kupitia programu aliyoianzisha ya HERNEEDS, amegundua uhitaji mkubwa wa taulo za kike kwa wanafunzi wa sekondari lakini bidhaa hiyo imekuwa ikiuzwa ghali na kufanya baadhi ya wanafunzi kushindwa kuimudu.
Arjun kwa kushirikiana na wahisani wa ndani na nje ya nchi hususani Dubai ameweza kununulia taulo za kike wanafunzi katika sekondari 33 zilizopo Arusha kupitia programu hiyo ya miaka mitatu.
Akizungumza na mwanafunzi huyo aliyekuwa ameongozana na baba yake Atul Mittal mkurugenzi wa Mount Meru Petroleum and Millers, Spika Tulia amesema kipaji alichokionesha Arjun ni kikubwa ambapo wanafunzi wengine wanapaswa kuiga.

Akijibu ombi hilo Spika Tulia amesema bidhaa hiyo imerudishiwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), kutokana na wafanyabiashara kuendelea kutoza gharama kubwa hata baada ya Serikali kuondoa kodi hiyo.
Spika Tulia amesema awali lengo la Serikali lilikuwa ni kuondoa kodi hiyo ili bidhaa hiyo ishuke gharama lakini pamoja na kuondolewa bado wafanyabiashara waliendelea kuuza kwa bei Ile Ile jambo ambalo sio sawa.
SOMA: Mazungumzo yafanyika kusaidia gharama taulo za kike
Aidha Dk Ackson amempongeza Mtanzania Arjun Kaur Mittal kwa kufanikiwa kuanzisha kampeni ya kugawa taulo salama za kike kwa wanafunzi kupitia programu ya hiyo na kumuahidi bunge lake kuwa litaendelea kuangalia uwezekano wa kuondoa kodi katika bidhaa hiyo ili iweze kuwafikia wengi.



