DAR ES SALAAM; NAIBU Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum, Mwanaidi Ali Khamis amesema mazungumzo baina ya wizara hiyo na Wizara ya Fedha yanaendelea katika kuhakikisha taulo za kike zinapatikana kwa gharama nafuu bila kodi, ili kuwezesha wanawake na wasichana wa kaya masikini kupata afua hiyo.
Pia amesema wataendelea kushughulikia changamoto za mila na desturi kandamizi zinazokwamisha jitihada za kumuinua msichana ikiwemo mimba za utotoni, ndoa na ukeketaji.
Akzungumza leo Dar es Salaam, Naibu Waziri huyo amesema “Mila, desturi na utamaduni kandamizi hufanya wasichana wakose kujiamini, kujitambua na kutotimiza ndoto zao hivyo, serikali itapendelea mzidi kutoa elimu kwa umma kuhusu athari za mila na desturi zenye madhara.”
Amesema kuwa suala la kuondolewa kwa kodi taulo za kike, mazungumzo yanaendelea na kwamba watahakikisha zinapatikana kwa gharama nafuu na zenye ubora unaotakiwa.
Khamis amesema utafiti uliofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kushughulikia Watoto wa mwaka 2021, kuhusu ukatili dhidi ya watoto unaonesha kuwa mvulana mmoja kati ya saba anakutana na ukatili wa kingono kabla ya miaka 18.
Kati ya watoto hao asilimia 71 wamefanyiwa ukatili wa kimwili. Hata hivyo, utafiti huo unaonesha kuwa watoto wa kike idadi ipo juu kwani msichana mmoja kati ya wasichana watatu amekutana na ukatili wa kingono kabla kutimiza miaka 18 na ni sawa na asilimia 72 wamekutana na ukatili wa kimwili.
Pia amesema takwimu za utafiti wa kidemografia wa Afya (TDHS) mwaka 2016 umeonesha kuwa asilimia 36 ya wasichana wenye umri kati ya miaka 20 hadi 24, waliolewa kabla ya kutimiza miaka 18 tatizo hilo kubwa zaidi vijijini huku mijini ikiwa na idadi ndogo.
Kuhusu hatua zinazochukuliwa na serikali, ameeleza kuwa wanasubiri marekebisho ya sheria ya ndoa 1971 ambayo inaruhusu mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 14 kuolewa kwa idhini ya wazazi au walezi, yataondosha mazingira ya kuwepo kwa mila wezeshi zinazochochea vitendo hivyo
“Hatua za kimaendeleo kuwezesha elimu kwa mtoto wa kike zinaendelea kwani Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia watoto wa kike waliokatishwa masomo kuendelea na masomo hivyo, niwatake msifanye mchezo kwenye fursa hizo kwani tupo tutawalinda nanyi muendelee na masomo,” amesisisitiza.
Amesema takribani wasichana 28,000 wamerejea shule baada ya kuacha masomo kwa sababu mbalimbali kati ya 2022/23.
Katika mwaka wa masomo, 2022 wanafunzi waliorejea shule ya msingi ni 9,379 sawa na asilimia 13.92 na wanafunzi sekondari ni 8,153 sawa na asilimia 12.94 wakati kwa mwaka 2023, wanafunzi waliorudi shule ni 5,057 wa shule ya msingi na sekondari ni 6,191 sawa na asilimia 18.7.
“Serikali inaendelea kuimarisha ubora na miundombinu ya elimu nchini kwani hadi sasa
shule 10 kati ya 26 zimejengwa kwa ajili ya wasichana lengo kuongeza ushiriki kwenye masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati,” amesema.
Comments are closed.