TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imekamilisha awamu ya kwanza ya udahili kwa ngazi ya shahada ya kwanza katika taasisi za elimu ya juu nchini kwa mwaka wa masomo wa 2022/2023 na kufungua awamu ya pili huku kukiwa na ongezeko la nafasi 7,267 ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa alibainisha hayo jana (Jumatano) wakati akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake, Dar es Salaam.
Dirisha la kwanza la udahili kwa mwaka huu lilifunguliwa Julai 8 na kufuatiwa na Maonesho ya 17 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yaliyofanyika Dar es Salaam Julai 18 hadi Julai 23 mwaka huu.
“Tume inatangaza kuwa awamu ya pili ya udahili wa shahada ya kwanza kwa mwaka wa masomo 2022/2023 imeanza rasmi leo Agosti 24 (jana) hadi Septemba 6, 2022,” alisema Profesa Kihampa.
Alihimiza waombaji 37,006 waliodahiliwa katika zaidi ya chuo kimoja katika awamu ya kwanza ya udahili mwaka huu, kuthibitisha udahili wao katika chuo kimojawapo kuanzia jana hadi Septemba 6, mwaka huu.
“Watumie namba maalumu ya siri iliyotumwa kwa ujumbe mfupi kupitia namba zao za simu au baruapepe walizotumia wakati wa kuomba udahili… Uthibitisho wa udahili ufanyike kupitia akaunti aliyotumia mwombaji wakati wa kuomba udahili,” alisema.
Kihampa aliwahimiza waombaji ambao hawakufanikiwa kutuma maombi au ambao hawakudahiliwa katika awamu ya kwanza kutokana na sababu mbalimbali, kutumia vizuri fursa ya sasa kutuma maombi yao katika vyuo wanavyotaka.
“Tume inazielekeza taasisi za elimu ya juu nchini kutangaza programu ambazo bado zina nafasi. Aidha, waombaji wa vyuo wanahimizwa kuzingatia utaratibu wa udahili kwa awamu ya pili kama inavyooneshwa kwenye kalenda ya udahili iliyo katika tovuti ya TCU (www.tcu.go.tz),” alisema.
Kwa mujibu wa Profesa Kihampa, katika awamu ya kwanza ya udahili, waombaji 106,295 walituma maomba ya kujiunga katika vyuo 76 vilivyoidhinishwa kudahili huku programu 757 zikiwa zimeruhusiwa kudahili ikilinganishwa na programu 724 zilizoruhusiwa katika mwaka wa masomo wa 2021/ 2022.
“Mwaka huu kuna nafasi 172,168 ikilinganishwa na nafasi 164,901 zilizokuwapo mwaka jana na hili ni ongezeko la nafasi 7,267, sawa na asilimia 4.4 katika programu za shahada ya kwanza,” alisema Kihampa.
Taarifa hiyo ya TCU ilibainisha kuwa, katika awamu ya kwanza ya udahili, waombaji 75,163 sawa na asilimia 70.71 ya waombaji wote wa udahili wamepata udahili vyuoni.
Profesa Kihampa alisema: “Mwenendo wa udahili wa awamu ya kwanza katika kipindi cha miaka mitano ya 2018, 2019 hadi 2022, 2023 unaonesha ongezeko kubwa la waombaji ikiashiria ongezeko la wahitimu wa kidato cha sita na wa stashahada.”