ARUSHA: WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo Profesa, Jamal Katundu kuhakikisha anawachukulia hatua stahiki watendaji wa wizara hiyo wanaofanya kazi kwa mazoea na kuacha kuwaonea haya.
Pia amesema hatakubali kuona miradi ya maji kwenye eneo moja ikitumia mabilioni ya fedha huku wananchi wakikosa maji ,huku akikisisitiza miradi chechefu zaidi ya 177 ikamilike kabla ya utekelezwaji wa miradi mingine mipya
Waziri Aweso ametoa agizo hilo kwenye mkutano wa kuwashukuru wadau wa sekta ya maji nchini, kwa mchango wao mkubwa wa hali na mali katika kuwezesha mafanikio yaliyopatikana, sambamba na kutoa fursa ya maoni ya mapendekezo ya rasimu ya Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka 2002 ya toleo la mwaka 2023 na mpango mkakati wa wizara.
Amesema licha ya mafanikio mengi yaliyofikiwa, lakini bado kuna baadhi ya watendaji katika baadhi ya maeneo lazima wakubali kubadilika na kusimama kama kiongozi kwa kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
Ametoa mfano wa baadhi ya maeneo mkoani Mbeya vijijini, baadhi ya watendaji wamepelekewa fedha zaidi ya Sh,milioni 300 ya mradi wa maji na kuamua kugawana, huku mradi ukitelekezwa
“Katibu Mkuu chukua hatua kwa wale wanaokwamisha miradi yetu au wanaofanya kazi kwa mazoea usionee mtu haya”
Awali Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Profesa,Jamal Katundu amesema kupitia kikao hicho cha siku mbili,wadau hao watajadiliana masuala mbalimbali yanayohusu sekta hiyo muhimu ya maji ikiwemo fursa na changamoto, pamoja na rasimu ya sera mpya ya maji.