WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso ameitaka Mamlaka ya Maji ya Jiji la Tanga kuhakikisha wanasimamia miradi ya fedha za hatifungani unakamilika kwa wakati lakini na kurudisha gawiwo la hisa kwa wananchi .
Rai hiyo ameitoa leo wakati ziara yake ya kutembelea Mradi wa kuboreshaji hali ya upatikanaji wa maji katika miji ya Tanga , Muheza na Pangani kwa fedha za hatifungani ya kijani ya Tanga Uwasa yenye thamani ya Sh bilioni 54.
“Simamieni miradi hii iweze kukamilika lakini na kuhakikisha wanahisa wanapata hisa zao kwa wakati ili kujenga imani ya uwekezaji waliofanya,”amesema Waziri Aweso.
Hata hivyo Mbunge wa Jimbo la Tanga Ummy Mwalimu amesema kuwa hatifungani ya kijani ya Tanga ni ushahidi tosha kuwa wananchi wanaweza kufanya uwekezaji wa miundombinu badala ya kutegemea serikali pekee.
“Hati fungani hii ni ya kwanza Kwa nchi za afrika hii inaonyesha kuwa wananchi wakishirikishwa wanaweza kufanya makubwa Kwa ajili ya maendeleo yao,”amesema Ummy Mwalimu.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Tanga Batlida Buriani ameishukuru serikali kwa namna ambavyo ilivyo peleka pesa mkoani humo Kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji kwenye maeneo mbalimbali ya mkoa huo.