AZIZ KI: Atakumbukwa kwa mengi Yanga

WAFUATILIAJI wa soka Tanzania, wengi wao watakumbuka utambulisho wa kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Stephane Aziz Ki uliofanyika usiku kwa nakshi nakshi za aina yake.

Ilikuwa saa 6:00 usiku juu ya alama, Julai 15, 2022 katika kurasa za mitandao ya kijamii za klabu hiyo, kupitia picha mjongeo ilimtambulisha Aziz Ki, picha hiyo iliishia kwa maneno ‘Stephane Aziz Ki is Green and Yellow’.

Nyota huyo mzaliwa wa Ivory Coast lakini asili yake Burkina Faso alisajiliwa na Yanga akitokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast kwa mkataba wa miaka miwili. Hiyo ilikuwa sababu ya kuchezea timu ya taifa ya Burkina Faso, aliitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa hilo kwa mara ya kwanza mwaka 2017 na ameendelea kuwa mchezaji muhimu katika timu hiyo.

Alicheza kwenye michuano mbalimbali ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON). Akiwa ASEC Mimosas aliojiunga nao mwaka 2021 alifanikiwa kushinda mataji mawili ya Ligi Kuu Ivory Coast mwaka 2021 na 2022.

Machachari yake uwanjani yaliwavutia viongozi wa Yanga na kuwa na sababu ya kumtazama kwa macho ya fursa. Alisajiliwa na Wanajangwani kwa mkataba wa miaka miwili, uliokoma mwaka jana kabla ya kuongeza miaka miwili mingine, hata hivyo ameondoka Yanga na kujiunga na Wydad Casablanca ya Morocco kabla ya mkataba wa mara ya pili kuisha.

Kilichofanyika, Yanga ilifikia makubaliano ya kumuuza nyota huyo kwenda Wydad kwa sababu ilimuhitaji kwa
haraka nyota huyo wa kimataifa kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia ya Klabu itakayofanyika Marekani, Juni
mwaka huu.

Katika michuano hiyo Wydad imepangwa Kundi G pamoja na Juventus ya Italia, Manchester City ya England na Al Ain ya Falme za Kiarabu (UAE). Tangu ajiunge Yanga, jina lake lilitajwa tajwa na lipocheza fainali Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2023, katika michuano hiyo kwa hatua zote atakumbukwa kwa mchango na uwezo wake wa kutengeneza nafasi za mabao pamoja na kufunga.

Kwa upande wa hamasa uwanjani Aziz Ki alikuwa na nafasi yake ya kipekee, mara nyingi akiwa benchi timu yake ikicheza hakutulia kwa hekaheka za kuwaelekeza wachezaji wenzake wafanye nini, hata timu yake ikifunga bao shangilia yake ilikuwa ya hisia kwelikweli.

Kama ni midadi basi haikuachika kwa nyota huyo machachari wa Burkina Faso, hiyo inadhihirisha aliipenda Yanga kwa moyo wa dhati. Ndiyo sababu wakati anaondoka Aziz Ki alifanya jambo la kiungwana kuwaaga Wanayanga kwa ujumla wao. Alisema kuagana kunauma kwani moyo wake umejaa uzito kuwasilisha taarifa ya kuondoka kwake kwenye klabu ya moyo wake.

Alieleza kuiaga Yanga ni zaidi ya kuondoka klabuni, kwani alifanisha na kuaga familia iliyomlea na kumjenga
na kuwa mchezaji alivyo leo. “Yanga imenipa kusudi, imenipa makazi ya pili na zaidi Yanga imenipa mke
mrembo,” alisema Aziz Ki alipowaaga Wananchi.

Aliongeza: “Huu si mwisho ni mwanzo mpya tu,Yanga itabaki ndani yangu, sehemu ya hadithi yangu na ya roho yangu mpaka tukutane tena, daima mbele, nyuma mwiko.” Namna hiyo ndivyo alivyoaga baada ya kuitumikia Yanga kwa misimu mitatu.

Ofa aliyopata Aziz Ki kwenda Wydad imezinufaisha pande zote, Yanga pamoja na yeye mwenyewe kutokana na kile ambacho atakuwa akilipwa kwa mwezi huko Morocco. Kwani makubaliano ya mshahara na timu yake mpya ni Dola za Kimarekani 27,000 kwa mwezi, kutoka Dola 13,000 alizokuwa akilipwa na Wananchi.

Yanga itamkumbuka kwa mengi Aziz Ki ikiwa ni pamoja na kumuuza mchezaji huyo kwenda Wydad kwa dau la Sh bilion 1.8.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button