Babu jela miaka 30 kwa kumnajisi mjukuu wake

MAHAKAMA ya Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza imemhukumu Lucas Maselele ,56, mkazi wa kijiji cha Lugata kutumikia kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mjukuu wake mwenye umri wa miaka 13 (jina limehifadhiwa).

Hukumu hiyo imesomwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Sengerema, Evod Kisoka katika kesi ya jinai namba 16492/2024.

Awali, Mwendesha Mashtaka, Wakili wa Serikali Nyamhanga Tissoro, aliieleza mahakama kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo mnamo Juni 4, 2024, katika kijiji cha Lugata Wilaya ya Sengerema Mahakama ilielezwa kuwa mshtakiwa alitumia mwanya wa mke wake kuwa msibani na kutekeleza unyama huo kwa mjukuu wake.

Hata hivyo, alifumaniwa na mkewe aliporejea nyumbani ghafla.

Baada ya tukio hilo, mshtakiwa alikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Juni 14, 2024, ambapo alikana mashtaka dhidi yake.

Upande wa Jamhuri uliwasilisha ushahidi wa kutosha kwa mahakama, na kesi hiyo iliendelea kusikilizwa hadi Machi 13, 2025.

Mahakama, baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote, ilizingatia ripoti ya daktari aliyemfanyia uchunguzi mtoto huyo pamoja na mashahidi waliotoa ushahidi thabiti dhidi ya mshtakiwa.

Mahakama ilijiridhisha kuwa upande wa Jamhuri umeweza kuthibitisha shtaka hilo bila kuacha shaka yoyote.

Kutokana na uzito wa kosa hilo na madhara kwa mtoto huyo, mahakama ilitoa hukumu ya kifungo cha miaka 30 jela kwa mshtakiwa. Aidha, mahakama ilieleza kuwa adhabu hiyo inapaswa kuwa fundisho kwa jamii ili kuzuia vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa watoto.

Kesi hii imeibua hisia kali miongoni mwa wakazi wa kijiji cha Lugata na Wilaya ya Sengerema kwa ujumla, ambapo wengi wamepongeza hatua ya mahakama kuhakikisha haki inatendeka.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button