Bajeti ya Tarura yaongezeka hadi bil 710/-

BAJETI ya uboreshaji wa miundombinu ya barabara za Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imeongezeka kutoka Sh bilioni 275 hadi Sh bilioni  710.

Taarifa hiyo imetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi, Zainabu Katimba wakati wa utiaji saini mkataba wa ujenzi wa Soko Kuu la Mwanga na Soko la Samaki la Katonga  katika Manispaa ya Kigoma.

Katimba amesema kwamba ongezeko hilo la bajeti ni sawa na  asilimia 158.18 ambapo zinaenda kutekeleza miradi mbalimbali nchini.

Advertisement

Aidha, amesema kuwa kutokana na mvua kubwa zilizonyesha maeneo mbalimbali ya nchi na kusababisha madhara makubwa kwenye miundombinu ya barabara kama vile mvua za El nino, kimbunga Hidaya.

“Mhe. Rais kwa kutambua kuwa barabara hizi zinaunganisha jamii zetu kwa kutoa huduma mbalimbali za kijamii na zinatumika kwenye usafirishaji wa bidhaa mbalimbali za biashara na kupelekea kukuwa kwa uchumi wetu aliongeza Bajeti ya dharura ya Tarura”.

Ameongeza kuwa serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali zenye lengo la kuboresha maisha ya wananchi na mojawapo ya hatua zinazochukuliwa ni kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji.

“Msingi wa maboresho haya ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2020 – 2025, kama inavyofafanuliwa katika aya ya 57 ukurasa wa 82”, ameongeza Katimba.