MWENYEKITai wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amesema kosa la mtu mmoja lisisababishe chombo cha habari kufungiwa na kunyimwa haki ya wananchi kupata habari.
Balile ameyasema hayo hivi karibuni jijini Dar es Salaam na kueleza kuwa suala la kufungia chombo cha habari kwa kosa la mtu binafsi si sahihi.
Amesema unakuta chombo cha habari kinajiendesha kwa misingi na maadili mazuri na kinafuata sharia, lakini mtu binafsi au kiongozi anaenda kufanya mahojiano kwenye kipindi fulani na anatoa maneno yasiyofaa, ambayo yanasababisha chombo cha habari kufungiwa.
“Ni vyema mtu binafsi akawajibika na kubeba lawama sio chombo cha habari, unapofungia chombo kwa kosa la mtu binafsi unawanyima wananchi kupata habari, mfano kuna watu wameweka matangazo yao unadhani chombo kikifungiwa wao watafikia vipi lengo lao la kutangaza?
“Pia itasababisha wafanyakazi kama madereva , wapishi nao kusababisha hata wanafunzi kukosa haki ya kupata habari kwa kosa la mtu mmoja.
‘Kama Mwandishi akifanya ndivyo sivyo aadhibiwe kwanza, kisha taratibu zingine za kufungia chombo cha habari zifuatwe,” amesema.
Balile ameongeza kuwa ili chombo kiwajibishwe ni lazima ufanyike uchunguzi, ili kujiridhisha kwamba chombo cha habari kimeunga mkono kilichofanywa na mtu binafsi, ambaye amesabanisha kuleta taharuki kwenye jamii.