BALOZI wa Tanzania nchini Ujerumani, Dk Abdallah Possi amesema wafanyabiashara wa Tanzania wana fursa ya kuuza mbogamboga na matunda katika soko la Ujerumani.
Balozi Dk Possi alisema hayo Jumatano kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanywa kwa njia ya video akieleza fursa na kazi zinazofanywa na ofisi ya ubalozi wa Tanzania nchini Ujerumani.
Ubalozi huo pia unatoa huduma za kibalozi kwa nchi za Poland, Cheki, Slovakia, Romania, Hungary na Bulgaria.
Balozi Dk Possi alisema kwa sasa soko la mbogamboga na matunda lina mwitikio mkubwa kwa sababu hata katika maduka ya bidhaa yakiwemo ya chakula, matunda kutoka Tanzania yapo.
“Fursa za biashara hususani ya mbogamboga na matunda ipo lakini pia hata la kahawa ya oganiki, ukienda dukani unakuta maparachichi ya Tanzania, hii ni fursa wafanyabiashara wetu kuchangamkia kwa kujiunga pamoja kwenye mnyororo wa biashara,” alisema.
Dk Possi alisema fursa nyingine kwa Tanzania ni utalii na kusema takwimu za Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) ya hivi karibuni zinaonesha kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza kuleta watalii Tanzania zimo Ujerumani na Poland.
“Tanzania inavutia zaidi kwenye utalii na ndio maana tumeweka mkazo zaidi kwenye sekta hii, mwishoni mwa mwaka jana tulifanya matukio ya kuhamasisha utalii kule Zurich, Uswisi na miji mingine ya Humbug na Oktoba mwaka huu tutafanya kule Colon, haya matamasha yanatangaza vivutio vyetu na watalii wanakuja kwa wingi Tanzania,” alisema.
Dk Possi alisema idadi kubwa ya watalii wanaokuja Tanzania wanachagizwa pia na uwepo wa usafiri wa moja kwa moja wa Shirika la Ndege la Eurowings kutoka Ujerumani kuja Tanzania.
Kuhusu kodi na tozo alisema nchi zinazoendelea zinatumia kodi kutoa huduma za jamii kwa wananchi wake na kuhimiza lazima kuwepo na wigo mpana wa walipa kodi na sio kutegemea wafanyakazi pekee ambao ni wachache ikilinganishwa na idadi ya wananchi.
Dk Possi alisema Tanzania na Ujerumani zina uhusiano mzuri na nchi hiyo ni wadau wakubwa wa maendeleo nchini kwa kufadhili na kutoa misaada na ushirikiano katika sekta mbalimbali zikiwemo za uhifadhi, elimu, afya na maji.
Kuhusu biashara, Balozi Dk Possi alisema hadi mwaka 2020 Tanzania ilikuwa imefanya biashara ya kuuza na kununua kutoka Ujerumani ya Dola za Marekani bilioni 2.38.
Aidha, taarifa za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), zinaonesha kuwa kuna jumla ya miradi 169 imeandikishwa yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 396 na miradi hiyo ikitekelezwa yote itatoa ajira kwa Watanzania 15,000.