Bandari Kwala kuhudumia makontena 823 kwa siku

BANDARI kavu ya Kwala iliyopo Vigwaza, Kibaha Pwani inatarajiwa kuhudumia shehena ya makasha 823 kwa siku.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alisema bandari ya Kwala inatarajiwa kuhudumia hadi makasha 300,395 kwa mwaka ambayo ni sawa na asilimia 30 ya makasha yote yanayohudumiwa na Bandari ya Dar es Salaam kwa sasa.
Msigwa alisema akiwa kwenye bandari hiyo Kibaha mkoani Pwani kuwa mpaka sasa ujenzi wa bandari hiyo umegharimu Sh bilioni 83.246.
Aliwaeleza waandishi wa habari baadhi ya kazi zilizofanyika ni kusafisha eneo la hekta 60 na ujenzi wa ukuta, kujenga yadi yenye ukubwa wa hekta tano kwa kiwango cha zege ambao tayari umekamilika kwa asilimia 100 ukigharimu Sh bilioni 36.670.
Msigwa alitaja kazi nyingine ni ujenzi wa reli ya mchepuko kilometa 1.3 kutoka stesheni ya Shirika la Reli Tanzania hadi Bandari Kavu ya Kwala kwa gharama ya Sh milioni 677.3.
Alisema moja ya sababu za serikali kuamua kujenga bandari kavu ya Kwala ni msongamano wa shehena bandarini. Hivyo kwa kujenga bandari hiyo, anaamini tatizo litatatuliwa kwa kiwango kikubwa.
“Bandari ndiyo imeanza na tayari imeshapokea makontena 700 na makontena 400 tayari yameshachukuliwa na nchi jirani,” alisema Msigwa.
Alisema sababu nyingine ya kujenga bandari hiyo ni za kiufundi kwa vile eneo ilipo ni miundombinu ya barabara kuu inayounganisha nchi jirani za Burundi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Malawi, Zambia na Uganda.
Alitaja faida zitakazopatikana kwenye matumizi ya bandari hiyo ni kuongeza ufanisi na kiasi cha shehena inayohudumiwa katika Bandari ya Dar es Salaam, kuongezeka kwa mapato ya serikali kupitia huduma zitolewazo katika Bandari za Dar es Salaam na Kwala.
“Pia itapunguza gharama za uendeshaji hivyo kuvutia wateja kutumia Bandari ya Dar es Salaam, kuongeza ushindani wa bandari ya Dar es Salaam kikanda ukizingatia uwekezaji wa bandari za nchi jirani katika bandari kavu,” alisema.
Aliongeza kuwa itaimarisha shughuli za kiuchumi na biashara za mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kwa kupunguza msongamano wa magari uliopo sasa.
Itaimarisha usalama barabarani kwa kuwa idadi kubwa ya shehena ya bandari ya Dar es Salaam itatumia usafiri wa reli.
“Faida nyingine tutakayopata ni kwamba miundombinu ya barabara za mikoa ya Dar es Salaam na Pwani itakuwa na maisha marefu lakini pia itaongeza ajira kwa wakazi wanaoizunguka bandari kavu ya Kwala na taifa kwa ujumla,” alisema



