“Barabara Kimara-Bonyokwa-Kinyerezi ikamilike haraka”

WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega ametembelea barabara ya Kimara – Bonyokwa – Kinyerezi yenye urefu wa kilometa 7 iliyopo mkoani Dar es Salaam na kusisitiza umuhimu wa kuharakisha ujenzi wa barabara hiyo ya kimkakati.
Katika ziara hiyo, Ulega ameagiza mkandarasi anayejenga barabara hiyo, kampuni ya Nyanza Road Works kuhakikisha kazi zinafanyika usiku na mchana ili kukamilisha haraka na ubora unaotakiwa.
“Kazi imeanza rasmi na wananchi wataanza kushuhudia maendeleo ya ujenzi wa barabara hii muhimu. Mkandarasi ahakikishe anakuwa na wafanyakazi wa kutosha na kwa ajira zisizo za ujuzi zitolewe kwa wananchi wa maeneo ya jirani na mradi ikiwemo Bonyokwa kama sehemu ya kurudisha kwa jamii,” amesema Ulega.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli ameunga mkono agizo hilo akisisitiza kuwa ajira za muda mrefu wakati wa ujenzi ni fursa kwa wananchi wa Bonyokwa, Kinyerezi, Kimara na maeneo jirani.
Barabara hiyo muhimu inatarajiwa kuwa kiunganishi kikubwa kati ya majimbo ya Ubungo na Segerea, hatua inayotarajiwa kuboresha huduma za usafiri na kuinua uchumi wa eneo hilo.
Waziri Ulega ameahidi kuwa serikali itasimamia mradi huo kwa weledi huku akiwahakikishia wakandarasi kuwa malipo yao ni kipaumbele cha serikali.
“Nyanza Road Works mmeonesha rekodi nzuri, tunawaamini, na tunategemea kazi bora zaidi katika mradi huu,” aliongeza.
Wananchi wanaoishi maeneo ambayo barabara hiyo inapita Kimara, Bonyokwa, Kinyerezi na maeneo jirani sasa wana matumaini makubwa ya kupunguza changamoto za miundombinu, usafiri na wanatarajia kunufaika kiuchumi kupitia mradi huu wa ujenzi.
Ujenzi wa barabara hiyo utajumuisha daraja lenye mita 25 na madaraja madogo saba ya kalvati na mkandarasi akitakiwa kufunga taa za barabarani.