WANANCHI wa mtaa wa Bunazi kata Kasambya wameondokana na changamoo ya barabara kujaa maji na kushindwa kupita baada ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) Wilaya ya Missenyi mkoani Kagera kutengeneza barabara ya njia nne kiwango cha lami.
Akizungumza mara baada ya kuweka Jiwe la Msingi kwenye mradi huo, Meneja wa Tarura Wilaya ya Missenyi Mhandisi Ally Maziku amesema kukamilika kwa barabara hiyo kumewezesha wananchi kupita kwa urahisi na kuondoa matengenezo ya mara kwa mara.
“Kutengenezwa kwa barabara hii kwa kiwango cha lami imewezesha wananchi kupita kiurahisi na kuleta faida kama kukua kwa shughuli za kiuchumi na kuondoa matengenezo ya mara kwa mara,” amesema Maziku.
Pia ameongeza kuwa kati ya kilomita tano zilizokusudiwa kutengenezwa kwenye wilaya hiyo, kilomita tatu zimeshakamilika na kwa matengenezo mradi wa njia nne umefikia asilimia 95 na sasa upo kwenye kipindi cha matazamio.
Veneritha Gambeye na Remigius Poul ni miongoni mwa wakazi wanaoishi mtaa huo ambapo wameeleza kuwa kabla ya matengenezo ya barabara hiyo ilikuwa ngumu kupitika hasa msimu wa mvua na muda mwingine walilazimika kuhama.
“Hii barabara imeleta unafuu kwasababu haya maeneo yalikuwa yanajaa maji njia ilikuwa haipitiki tunaomba msaada wa kuvushwa na muda mwingine tunahamia kwa ndugu zetu mpaka maji yapungue ila baada ya kutengenezwa maji yamepungua kwa kiasi kikubwa”. Wamesema wakazi hao.
Mbunge wa Jimbo la Nkenge, Frolence Kyombo ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuongeza kiwango cha bajeti ya ujenzi wa miundombinu ya barabara kwani imesaidia kutatua changamoto za wananchi wakati wa kusafiri na kusafirisha bidhaa zao.
“Ndani ya Wilaya ya Missenyi kipindi cha nyuma bajeti ya barabara ilikuwa ni Sh milioni 700 tu, lakini hivi sasa tunapata bilioni 2.4 kwa mwaka,”amesema Kyombo.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Godfrey Eliakimu Mnzava ameridhishwa na utekelezaji wa mradi huo na kuweka Jiwe la Msingi na kuipongeza Tarura Missenyi kupitishwa mfumo wa manunuzi kidigitali.
“Mwenge wa Uhuru umeridhika kuwa kazi imefanyika vizuri na Mwenge wa Uhuru utaweka Jiwe la Msingi katika mradi huu wa ujenzi wa barabara na niwapongeze Tarura Wilaya ya Missenyi kuzingatia mfumo wa manunuzi wa kidigitali,” amesema Mnzava
Barabara ya njia nne ya urefu wa kilomita 0.5 iliyowekewa jiwe la msingi na kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru kitaifa utekelezaji wake ulianza Septemba 19, 2023 na kukamilika kwa 95% Machi 13, 2024 kwa gharama za Sh milioni 186.