Wananchi 150,000 wanufaika kituo cha kupoza umeme

GEITA: ZAIDI ya wananchi 150,000 katika Mkoa wa Geita wanapata huduma ya umeme, ikiwa ni ongezeko kubwa kutoka wateja takribani 1,500 wa awali, hatua inayotokana na uboreshaji wa miundombinu ya usambazaji umeme.
Hayo yamebainishwa leo na Aprili 17, 2026 na Meneja Tanesco Mkoa wa Geita, Mhandisi Michael Mbwana wakati Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenan Kihongosi alipotembelea mradi wa kituo cha kupokea na kupooza umeme Mpomvu-Geita.

Mradi huo ulizinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Oktoba 15 mwaka 2022 ukilengo kuboresha upatikanaji wa nishati ya umeme wa wananchi wa Geita.
Akizungumza baada ya kutembelea mradi huo, Kihongosi amesema maendeleo ya taifa lolote yanatokana na uwepo wa nishati ya uhakika ya umeme, kwani ni nyenzo muhimu katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo.
Kihongosi amesema mradi huo ni mkombozi kwa Mkoa huo huku akimpongeza Rais Samia kwa uwekezaji huo mkubwa hali iliyoimarisha upatikanaji wa umeme mkoani humo.

“Sera ya CCM ni kuhakikisha vijiji na vitongoji vyotr vinafikiwa na umeme nchini, Chama tutaendelea kuisimamia serikali ili kuhakikisha inafikisha umeme maeneo yaliyobakia,” amesema Kihongosi.
Awali, akitoa taarifa ya maboresho ya mradi huo Mbwana ameeleza kuwa hadi kufikia Machi 30, mwaka huu mkoa una jumla ya wateja 154,094 ambao kati ya hao wa matumizi ya kawaida ni 106,961, wadogo wa majumbani ni 46,868, viwanda vya kati 145, wateja wakubwa 29 na matumizi ya shirika nane.

Amesema ujio wa mradi huo katika Mkoa huo umeleta chachu ya maendeleo kwa wananchi wa eneo hilo na umekuwa kichocheo kwa wawekezaji wakubwa.
“Hali ya usambazaji umeme kwenye Mkoa wa Geita imeendelea kuimarika hasa kutokana na kuendelea kwa utekelezaji wa miradi kabambe ya kusambaza umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Tanesco,” amesema Mbwana
Ameongeza; “Mpaka sasa vijiji 486 kati ya 486 vishapelekewa umeme ambavyo ni sawa na asilimia 99,
Pia vitongoji 1,193 kati ya 2,195 vimekwisha kupelekewa umeme sawa na asilimia 54”.



