ADDIS ABABA: Mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Afrika (AU) unaofanyika nchini Ethiopia mwishoni mwa wiki hii utajadili ajenda mbalimbali, ikiwemo mzozo wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Leo, Baraza la Usalama la AU litakutana kujadili mzozo huo, ambapo waasi wanaoungwa mkono na Rwanda wamedhibiti maeneo kadhaa mashariki mwa DRC.
Asasi ya kimataifa inayoshughulikia mizozo, ICG, imesema mzozo huu unahatarisha kuleta makabiliano kati ya mataifa mengi ya kanda ya maziwa makuu.
Umoja wa Afrika umeithibitisha kuwa viongozi wote wakuu watashiriki kwenye mkutano wa Baraza la Usalama. SOMA: Congo yatoa shukrani mkutano wa SADC.EAC
Hata hivyo, Rais Felix Tshisekedi wa DRC hatoshiriki kikao hicho, amemtuma Waziri Mkuu Judith Suminwa Tuluka kumwakilisha. Tshisekedi anahudhuria mkutano wa kimataifa wa usalama mjini Munich na atafika Addis Ababa kwa mkutano wa kilele wa AU.Bado haijafahamika kama Rais Paul Kagame wa Rwanda atahudhuria kikao hicho.
Serikali ya Rwanda inakosolewa kwa kusaidia waasi wa M23, ambao hivi sasa wanadhibiti mji wa Goma na wanakielekea mji wa Bukavu.
Nchi za Afrika Mashariki zilifanya mkutano mjini Dar es Salaam, zikisisitiza kusitishwa kwa mapigano na kuanzishwa kwa mazungumzo na makundi ya waasi.