Baraza la Vyama: Wanasiasa wasipotoshe kura ya mapema Z’bar

TUME ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imepuliza kipenga cha kuanza kampeni za vyama vya siasa za takribani siku 40, zikihusisha ya vyama vya siasa 11 vilivyokidhi vigezo na sifa za kushiriki uchaguzi huo Zanzibar.
Kwa nyakati tofauti, viongozi wa vyama vya siasa wamekumbushwa majukumu yao kuhakikisha wanatumia majukwaa ya siasa kunadi sera za vyama zinazotokana na ilani za vyama vyao.
Akizungumza na waaandishi wa habari, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Ali Khatib anasema Uchaguzi Mkuu ni nafasi muhimu kwa vyama kunadi sera zinazotokana na ilani ya uchaguzi kuwashawishi wapigakura kufanya uamuzi sahihi.
Anawataka viongozi wa vyama vya siasa waliopewa jukumu la kupeperusha bendera za vyama vyao katika Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2025 kutumia vizuri majukwaa ya mikutano ya hadhara kuwaunganisha wananchi, badala ya kuwagawa.
SOMA: Msajili ataka wanasiasa watii sheria
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, uzoefu unaonesha katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu hususani Zanzibar, hujitokeza ugonjwa wa misuguano inayotokana na kauli za chuki na uhasama za baadhi ya wanasiasa.
“Siasa za aina hiyo sasa zimepitwa na wakati, kwa sababu asilimia kubwa ya wakazi wa Zanzibar ni vijana na hao
wanataka kuhakikishiwa nini watafanyiwa na vyama hivyo, hususani masuala ya maendeleo,” anasema.
Anasema vijana wanakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa ajira na uchaguzi ni nafasi nzuri kwa wagombea kuwaeleza watawafanyia nini endapo watachaguliwa na kushika madaraka.
“Moja ya changamotoinayolikabili taifa letu ni tatizo la ajira. Huu ni wakati mwafaka wa wagombea wa vyama vya siasa kuelezea wananchi likiwemo kundi la vijana kuwa wakipewa ridhaa kushika dola watawafanyia nini,” anasema.
Khatib ambaye pia ni mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha ADA- Tadea anawataka wagombea kujiepusha na kauli za matusi, ikiwemo za kashfa dhidi ya viongozi waliopo madarakani. Anasema wanachotakiwa kufanya ni kuonesha wanachotarajia kuwafanyia wananchi endapo watachaguliwa.
Alisema si uungwana kwa wagombea Wazanzibari kutumia majukwaa ya kampeni kwa ajili ya uchaguzi kukashifu, kuwakejeli wala kuwadhihaki viongozi waliopo madarakani. “Wagombea wote tunatakiwa kutumia majukwaa ya vyama vya siasa kutangaza sera zetu na si kutoa kauli za kejeli kwa viongozi waliopo madarakani,” anasisitiza.
Aidha, anawataka wanasiasa kutopotosha jamii kwa kusema kura ya mapema ni kinyume cha sheria na kwamba wataipinga. Anasema kauli kama hizo si sahihi kwa kuwa hazilengi kujenga umoja, mshikamano na amani kwa jamii, bali zinalenga kuhamasisha wananchi kufanya vurugu za kisiasa katika siku ya upigaji wake, jambo ambalo halikubaliki kwa kuwa ni hatari.
Khatib anasema kura ya mapema ipo kwa mujibu wa sheria iliyopitishwa na Baraza la Wawakilishi Mwaka 2018, ikilenga kutoa nafasi kwa watendaji wa ZEC na vikosi vya ulinzi kupata haki ya kushiriki uchaguzi kwa kupiga kura kabla ya kura ya watu wote.
“Wapo baadhi ya viongozi wakubwa wanatoa kauli za aina hiyo kwamba kura ya mapema haipo kihalali na wao wataipinga… Hii si kauli nzuri kwakuwa wanajua kabisa kwamba kura ya mapema ipo kwa mujibu wa sheria,” anasema Khatib.

Kauli ya Dk Mwinyi
Wakati akichukua fomu ya kuomba uteuzi wa kugombea urais wa Zanzibar, Mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Mwinyi anaweka bayana na kusisitiza suala la amani katika kipindi chote cha kampeni hadi kumalizika mchakato wote wa Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.
Anasema CCM itahakikisha inafanya kampeni zake kisayansi zaidi kwa njia ya kistaarabu, huku viongozi wake wakitakiwa kuelezea ilani ya CCM kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kwamba chama kitafanya nini kipindi cha miaka mitano hadi 2030.
Anasema Wazanzibari wamechoka kufanya uchaguzi wenye sura ya uhasama, chuki na wananchi kugawanyika, hali ambayo ni hatari kwani inasababisha kuzuka vurugu za kisiasa. Kwa mujibu wa Dk Mwinyi, upo uwezekano mkubwa wa kufanya uchaguzi kwa amani na utulivu kwa kujenga mshikamano na kuwaunganisha wananchi wote bila ya kuacha makovu na maumivu.
Anasema, “Hapa nazungumza nikiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwamba, matarajio yangu makubwa ni kuona mwaka huu tunafanya uchaguzi huru na haki; unaowaunganisha wananchi wote bila kuacha athari za maumivu na makovu ya majeruhi ya kisiasa…Tunaweza kufanya uchaguzi bila ya vurugu wala kugombana, inawezekana kabisa!”

Mgombea wa ACT- Wazalendo
Mgombea urais wa Zanzibar kupitia ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman anaahidi kufanya kampeni zinazonadi ilani ya chama hicho inayolenga kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi. Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, anasema anaamini Wazanzibari wana uwezo wa kufanya uchaguzi huru na haki usiokuwa na vurugu za kisiasa.
Anasisitiza uzingatiaji wa sheria zikiwamo za uchaguzi pamoja na sheria za ZEC akisema zinapaswa kuheshimiwa, kulindwa na kutekelezwa.
“Chama cha ACT-Wazalendo kimejipanga kufanya kampeni zenye kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi na maendeleo kwa wananchi wa Zanzibar,” anasema Othman katika mazungumzo na waandishi wa habari baada ya kurejesha fomu ya kuomba uteuzi wa kugombea.
Mwenyekiti wa ZEC
Mwenyekiti wa ZEC, Jaji George Kazi anasema tume imejipanga kikamilifu kuhakikisha inasimamia mchakato wa uchaguzi ulio huru na haki utakaotimiza matakwa ya wananchi kidemokrasia.
Anasema ZEC imekamilisha taratibu mbalimbali muhimu kwa ajili ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu ikiwa ni pamoja na kuandikisha wapigakura katika daftari la kudumu na kufanya uhakiki wa majina yao.
Jaji Kazi anasema mchakato wa pili ni kufanya uteuzi wa majina ya wagombea mbalimbali ikiwemo wa nafasi ya urais wa Zanzibar. Kazi hiyo tayari imefanyika, wagombea wa vyama 11 wameidhinishwa kwa ajili ya kinyang’anyiro hicho.
Mwenyekiti huyo anawataka wagombea wa nafasi ya urais kufanya kampeni za kistaarabu kwa kutumia majukwaa ya kampeni kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka huu kunadi sera zitakazoshawishi wapigakura kuwachagua na vyama vyao.
Anawataka wagombea kuacha kutoa kauli ambazo ni kinyume cha sheria, kuacha kupotosha jamii na kuepuka kuhamasisha vurugu za kisiasa. “Yupo mgombea ambaye anafahamu vizuri sheria zote lakini anawaambia wananchi kwamba kura ya mapema haipo kwa mujibu wa sheria… Kauli hizi ni sehemu ya viashiria vya uvunjifu wa amani,” anasema Jaji Kazi.
Anawataka wagombea wote kuhakikisha wanazingatia, wanaheshimu, wanatekeleza na kusimamia miongozo na Kanuni za Maadili katika Uchaguzi Mkuu wa 2025 zilizosainiwa na viongozi wa vyama hivyo wakilenga kufanya siasa za kistaarabu zinazozingatia amani na utulivu wa nchi.”