Bashe aagiza Dk Msolla akamatwe

WAZIRI wa Kilimo, Hussein Bashe ameagiza kukamatwa na kuhojiwa Meneja Masoko wa Kampuni ya mbolea ya Minjingu, Dk Mshindo Msolla kwa tuhuma za kukutwa na mifuko 776 ya mchanga katika ghala la kampuni ya mbolea ya Minjingu.

Maagizo ya Bashe yanaenda sambaba na kukamatwa kwa msimamizi wa ghala la mbolea ya Minjingu Mkoa wa Njombe na Meneja wa Kanda wa Nyanda za Juu Kusini wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Michael Sanga kwa tuhuma hizo.

Imeelezwa kuwa huenda mifuko hiyo 776 ya mchanga inatumika kuchakachua mbolea inayouzwa na kampuni hiyo. Bashe amesema hiyo ni hujuma ambayo haivumiliki, na atahakikisha wahusika wote wanachukuliwa hatua.

Ametoa agizo hilo baada ya wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Njombe kwa kushirikiana na wale wa kamati ya siasa ya mkoa huo, wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Antony Mtaka kufika katika ghala hilo na kukuta shehena ya mifuko ya mchanga katikati ya mifuko ya mbolea ya Minjingu.

Habari Zifananazo

Back to top button